Mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Lucas Pérez, ameweka wazi
historia yake ya maisha yenye machungu ya utotoni, akieleza jinsi wazazi wake
walivyomtelekeza akiwa na umri wa miaka miwili na sasa wanavyodai usaidizi wa
kifedha kutoka kwake.
Katika mahojiano ya hivi majuzi na El Partidazo de COPE, Pérez alisimulia kwa uchungu jinsi alivyoachwa katika makazi ya watoto yatima na wazazi wake, hali iliyomfanya alelewe na nyanya na babu yake.
"Nilipokuwa na miaka miwili, wazazi wangu waliniacha. Sikuwahi kuwaona tena mpaka ninapokuwa mtu mzima. Ilikuwa ni nyanya na babu walionitunza na kunilea," alisema Pérez.
Kwa mujibu wa mchezaji huyo ambaye sasa anachezea PSV Eindhoven, wazazi wake wamejitokeza tena maishani mwake baada ya yeye kupata mafanikio makubwa katika soka, wakimtaka awahudumie kifedha maisha yao yote.
"Sasa wananitaka niwape pesa kwa maisha yao yote. Walikuwa wapi nilipowahitaji? Siwezi kuelewa jinsi mtu anavyoweza kumwacha mtoto wake na kisha kumrudia miaka mingi baadaye kwa sababu ana pesa," aliongeza kwa uchungu.
Pérez pia alifichua kuwa mgogoro huu wa kifamilia ulikuwa moja ya sababu kuu zilizomfanya aondoke Deportivo La Coruña na kujiunga na PSV Eindhoven katika dirisha la usajili la Januari 2025.
"Watu wengi walifikiri niliondoka kwa sababu ya pesa, lakini ukweli ni kwamba nilihitaji mabadiliko kwa sababu ya hali yangu ya kifamilia. Nilikuwa napitia kesi ya kisheria dhidi ya baba yangu, na klabu haikunisaidia kwa namna yoyote," alisema mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36.
Pérez, ambaye aliwahi kucheza kwa klabu kama Arsenal, West Ham, na Alavés, amesema kuwa changamoto alizopitia maishani zilimjenga kuwa mtu mwenye nidhamu na mwenye kuthamini kila kitu alichonacho.
"Nimejifunza kuwa maisha ni magumu, lakini siwezi kuruhusu machungu ya zamani yanizuie kufanikiwa. Nimefanya kazi kwa bidii kufika hapa nilipo, na nitahakikisha ninatumia nafasi hii kusaidia wale walionijali tangu mwanzo," alihitimisha.
Kwa sasa, mshambuliaji huyo anaendelea na maisha yake mapya nchini Uholanzi, akijaribu kusahau machungu ya zamani na kuzingatia taaluma yake ya soka.