
McCarthy alituhumu klabu ya Gor Mahia na Tusker FC kwa kukosa kuwaachilia wachezaji wao kwa ajili ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Gambia na Gabon.
Klabu ya soka ya Gor Mahia imetoa majibu kufuatia madai hayo yaliyotolewa na kocha mkuu wa Harambee Stars kupitia mkurugenzi mtendaji Raymond Oruo imejitenga na kauli hiyo.
Katika majibu yake, Oruo alitetea msimamo wa klabu, akisisitiza kuwa walifuata kanuni za kuachilia wachezaji kwa ajili ya majukumu ya kimataifa.
Vilevile alieleza kuwa klabu ilifuata taratibu zote kwa mujibu wa sheria, na wachezaji wao waliungana na timu ya taifa mara tu baada ya mechi yao dhidi ya Bandari kukamilika.
"Nimeona taarifa ya kocha mkuu wa Harambee Stars baada ya mechi dhidi ya Gabon. Kocha na FKF wanajua vyema kanuni zinazohusu kuachilia wachezaji kwa majukumu ya kimataifa. Klabu zetu hazipaswi kutendewa kwa njia tofauti," Oruo alieleza.
Aliongeza kuwa kocha alipata fursa ya kuwafuatilia wachezaji wa Gor Mahia katika mechi ya ushindani dhidi ya Kariobangi Sharks na alipaswa kufanya maamuzi yake kulingana na hilo.
"Wachezaji wetu walikuwa tayari mara tu baada ya mechi dhidi ya Bandari. Ikiwa kocha aliamua kuwa hawahitajiki kwenye kikosi chake, basi anapaswa kusema hivyo wazi kwani alikuwa na nafasi ya kuwaona katika mechi ya ligi," aliongeza.
Oruo alihitimisha kwa kusisitiza kuwa Gor Mahia itaendelea kuunga mkono juhudi za timu ya taifa, "Klabu itaendelea kusaidia jitihada za timu ya taifa." alisema.
Kocha mkuu wa timu ya taifa Harambee Stars McCarthy alikua amesema kwamba vilabu vya Gori Mahia na Tusker walikuwa wameomba kubakisha wachezaji wao na walikubalina kuhusu hilo.
"Wachezaji waliopatikana wakati huo ndio niliowachagua. Gor Mahia na Tusker waliomba ruhusa ya kuwabakisha wachezaji wao, na tulikubaliana. Lakini siwezi kuchagua wachezaji ambao sijawaona wakicheza au ambao siwajui, ndiyo maana hakuna aliyekuwa kwenye kikosi," McCarthy alisema baada ya mechi ya Jumapili.