
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, alithibitisha siku ya Jumatatu kuwa Bukayo Saka alikuwa amepona kabisa na alikuwa tayari kurejea uwanjani.
Winga huyo alianza mechi akiwa benchi katika pambano la Ligi Kuu ya Uingereza dhidi ya Fulham lakini aliingizwa uwanjani dakika ya 66, akichukua nafasi ya Ethan Nwaneri.
Chini ya dakika saba baadaye, alifunga bao kwa kichwa kutoka umbali mfupi baada ya kupokea pasi maridadi kutoka kwa Gabriel Martinelli.
Saka alisherehekea kwa tabasamu pana huku mashabiki wakimshangilia kwa sauti kubwa uwanjani.
Baada ya kusherehekea na wachezaji wenzake, alikimbia kuelekea benchi kushiriki furaha hiyo na Sam Wilson, kocha mkuu wa mazoezi ya utimamu wa mwili wa Arsenal.
Wilson alihusika pakubwa katika kuhakikisha Saka anarejea
uwanjani akiwa katika hali bora.
Urafiki kati ya Saka na Wilson umeendelea kwa miaka kadhaa, kwani wawili hao walifanya kazi pamoja wakati Saka alipokuwa katika kikosi cha Arsenal cha wachezaji wa chini ya miaka 21.
Ishara yake ya kushukuru siku ya Jumatatu usiku iliangazia kazi kubwa inayofanywa nyuma ya pazia, siyo tu na wachezaji, bali pia na benchi la ufundi.
Wakati Saka akiingia uwanjani, Arsenal tayari ilikuwa
inaongoza 1-0, kutokana na bao la Mikel Merino lililoguswa na beki wa Fulham na
kujaa wavuni katika kipindi cha kwanza.
Rodrigo Muniz aliifungia Fulham bao la kufutia machozi, lakini Arsenal walidhibiti mchezo na kushinda 2-1.
Ushindi huo muhimu uliwapeleka Arsenal hadi alama 61, ingawa bado wako nyuma kwa pointi tisa dhidi ya Liverpool, ambao wana alama 70.
Baada ya kumaliza katika nafasi ya pili kwa misimu miwili
iliyopita, itasubiriwa kuona kama Arsenal wataweza kupunguza pengo na kuwania
ubingwa msimu huu.