
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Michezo wa Arsenal, Edu Gaspar, ametoa ujumbe wa kuaga rasmi klabu hiyo, akifunga ukurasa wa miaka mitano na nusu ya kujivunia katika historia yake ya taaluma ya soka.
Edu, ambaye alijiunga na Arsenal mwezi Julai mwaka 2019 kama Mkurugenzi wa Kiufundi, alihitimisha rasmi kandarasi yake jana, Aprili 11, 2025, baada ya kuwa likizoni tangu Novemba 2024 alipoondoka rasmi kazini.
Katika taarifa aliyotoa Alhamisi kupitia mitandao ya kijamii, Edu alielezea shukrani zake kwa klabu, wachezaji, mashabiki na kila mmoja aliyeshiriki katika safari yake ya kuijenga upya Arsenal.
"Kwa moyo uliojaa shukrani, leo nafungia rasmi mmoja wa sura muhimu zaidi katika taaluma yangu. Baada ya miaka mitano na nusu, safari yangu kama Mkurugenzi wa Michezo wa Arsenal FC imefikia kikomo," alisema Edu.
Edu alielezea jinsi alivyopewa jukumu la kuhakikisha Arsenal inarejea katika hadhi yake ya zamani ya ushindani na mafanikio, akisisitiza kuwa kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya kilipaswa kuwa kiwango cha chini kwa klabu ya ukubwa kama Arsenal.
"Nilijiunga na klabu nikiwa na dhamira ya kuirejesha Arsenal miongoni mwa vigogo wa soka, kuleta mabadiliko ya kiutamaduni, kushindania mataji, na kuhakikisha kufuzu kwa Ligi ya Mabingwa linakuwa jambo la kawaida," alisema.
Edu pia alikumbuka kwa fahari jinsi alivyoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Michezo wa kwanza katika historia ya klabu, akisema ilikuwa heshima kubwa kwake.
Hakusahau mchango mkubwa wa mashabiki, akisema walikuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya mabadiliko ya Arsenal.
"Kwa mashabiki wetu, asanteni kwa moyo wote! Mlioleta nishati, msisimko, na uhusiano wa kipekee kila mechi. Emirates iligeuka kuwa kama toleo jipya la Highbury!" alisema.
Aliwashukuru wamiliki wa klabu Stan na Josh Kroenke, meneja Mikel Arteta, benchi la ufundi, bodi ya wakurugenzi, wachezaji, na wafanyakazi wote wa klabu kwa ushirikiano na ukarimu alioupata.
"Haikuwa rahisi, lakini kazi yetu ya pamoja na roho ya umoja ilinifanya nijihisi kutosheka kwa miaka yote hii," aliongeza.
Edu pia alituma salamu za heri kwa mrithi wake, Andrea Berta, ambaye ameteuliwa rasmi kuchukua nafasi hiyo nyeti ya michezo katika klabu hiyo ya London.
"Ninaondoka nikiwa na moyo wa amani na fahari kubwa kwa kile tulichokijenga pamoja. Nawatakia kila la heri Arsenal FC!"
Edu alisisitiza kuwa alisubiri hadi
siku ya mwisho rasmi ya mkataba wake ili kutoa taarifa hiyo, akiheshimu klabu
na watu wote waliohusika.