logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Je, Uganda ndio yenye mashabiki kindakindaki wa Arsenal duniani?

Mashabiki wa Arsenal waliwahi kukamatwa nchini Uganda kwa kufanya maandamano ya ushindi baada ya kuifunga Man United.

image
na BBC NEWS

Football20 April 2025 - 09:49

Muhtasari


  • Vilabu vya England, vina mashabiki kote Uganda. Hadi kupitia makundi ya WhatsApp ili kuendeleza mijadala zaidi, mbali na katika kumbi na baa.
  • Baadhi wanasema ushabiki wa uadui upo zaidi kwa mashabiki wa Arsenal na Man Utd wa Uganda. Wanasema hilo linatokana na umri na historia.

Mwaka 2023, kundi la mashabiki wa Arsenal walikamatwa nchini Uganda kwa kufanya maandamano ya ushindi baada ya kuifunga Manchester United

Mashabiki wa Arsenal nchini Uganda walifanya sherehe ya usiku hadi kukaribia alfajiri wiki hii, nje ya kumbi za kuonesha michezo na baa kote Uganda, baada ya timu yao kupata ushindi dhidi ya Real Madrid.

Timu hiyo yenye maskani yake kaskazini mwa London ilishinda 3-0, nyumbani, katika mkondo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Kila klabu hiyo inapocheza, taifa hilo la Afrika Mashariki husimama. Sambamba na Manchester United; ni timu za Ligi Kuu ya England (EPL) zenye mashabiki wengi Uganda.

Ibada za kanisani, zilizojaa mashabiki waliopambwa na rangi nyekundu na nyeupe za The Gunners, hufanyika kabla ya mechi kubwa.

Ushabiki kwa Arsenal na vilabu vingine vya Uingereza huonekana kote Uganda, huku maduka na wafanya biashara wadogo wadogo wakiuza jezi na makampuni makubwa yakifanya matangazo, na kampuni za kamari zikifanya biashara kubwa.

"Nimeripoti soka kote barani Afrika kwa miaka mingi na naweza kukuambia, ushabiki wa soka nchini Uganda uko katika kiwango kingine," anasema mwanahabari mkongwe wa michezo Isaac Mumema.

Kwa Swale Suleiman, fundi na shabiki wa Manchester United niliyekutana naye kwenye gereji moja katika mwa mji mkuu, Kampala, msisimko upo katika ukweli kwamba mechi za EPL ni za ushindani, za kuburudisha na wakati mwingine hazitabiriki na hata "timu ndogo inaweza kusababisha tafrani."

Vilabu vya England, vina mashabiki kote Uganda. Hadi kupitia makundi ya WhatsApp ili kuendeleza mijadala zaidi, mbali na katika kumbi na baa.

Lakini mashabiki wa Arsenal wanaonekana kuupeleka ushabiki wao katika kiwango kingine – kiasi cha wengine kukamatwa kwa kufanya maandamano ya ushindi bila taarifa ya polisi baada ya kushinda mechi kubwa.

Hata hivyo, aina hii ya ushabiki pia ina upande mbaya, mapenzi ya mchezo huu wakati mwingine hugeukia kuwa vurugu mbaya.

"Waganda wanapenda sana mpira wa miguu," anasema mwenyekiti wa Chama cha Makocha wa Soka Uganda (UFCA) Stone Kyambadde.

"Ushabiki huu wa soka umeongezeka zaidi kwa vijana kwa sababu wanatazama Ligi Kuu ya England popote walipo," anasema.

Wanaweza kufuatilia kupitia simu zao, lakini hasa ni kupitia matukio ya kukusanyika hata katika vijiji vya mbali, kunakuwa na ukumbi na televisheni ambapo mashabiki hukusanyika kutazama mechi.

Nyakati za vilio

Kuna nyakati za majonzi. Wanakijiji karibu na Ziwa Victoria walikusanyika Desemba mwaka jana, kumzika seremala mwenye umri wa miaka 30, aliyeuawa kwa kupigwa risasi wakati wakishangilia ushindi wa Arsenal dhidi ya Manchester United.

John Senyange alikuwa akitazama mechi katika ukumbi wa video katika mji wa Lukaya – pale shangwe zilipolipuka kutoka kwa mashabiki wa Arsenal baada ya filimbi ya mwisho, shangwe hizo ziliwakasirisha wapinzani wao, akiwemo mlinzi, ambaye inasemekana alifyatua risasi.

Mapema msimu huu, umbali wa kilomita 300 (maili 186) katika eneo la kusini-magharibi mwa Kabale, shabiki wa Manchester United, Benjamin Ndyamuhaki aliuawa kwa kuchomwa kisu na shabiki wa Arsenal baada ya wawili hao kuzozana kuhusu matokeo ya pambano kati ya Arsenal na Liverpool.

Mwaka 2023, kulikuwa na vifo vinne vinavyohusiana na Ligi Kuu ya England, katika maeneo tofauti ya nchi - mashabiki wawili wa Arsenal waliuawa na wafuasi wa Man Utd, shabiki mmoja alikufa katika mazingira ya kushangaza baada ya Man Utd kulazwa 7-0 na Liverpool na mtu mwingine alikufa kutokana na majeraha ya kuchomwa kisu baada ya kujaribu kuingilia kati mapigano baada ya Arsenal kushindwa na Man Utd.

Vurugu za soka nchini Uganda zilianza miaka ya 1980. Michezo ya ndani ilikuwa na sifa ya kurushiana mawe na ngumi kati ya mashabiki pinzani.

"Mara zote kumekuwa na visa vya vurugu wakati Express FC na SC Villa - timu mbili kuu nchini Uganda – zinapocheza dabi," anasema mchambuzi wa michezo Lumbuye Linika.

Kamari yalaumiwa

Lakini mambo yamekuwa mabaya kutokana na uchezaji wa kamari. Mashabiki wengi wanajaribu kujipatia riziki kwa kuweka pesa zao huko.

Katika kisa cha kusikitisha miaka kadhaa iliyopita, polisi walisema mtu mmoja alijiua kwa sumu baada ya kupoteza pesa katika kamari ya mpira.

"Mashabiki wengi wa kandanda wanageukia kamari kama njia ya kupata pesa za haraka," anasema Amos Kalwegira, mkaazi wa Kampala, aliyesimama kuzungumza nami kwenye barabara ya Kampala nilipomwona akiwa na shati ya Man Utd.

"Huu umekuwa uwekezaji mkubwa wa kihisia ambao mara nyingi hubadilika kuwa ugomvi pale matokeo ya soka yanapokuwa mabaya."

"Soka inapaswa kutufurahisha. Soka ya Magharibi inapaswa kuwa aina ya burudani lakini hapa Uganda tumeigeuza kuwa njia ya kujitafutia riziki, na kuharibu furaha," anasema.

Collins Bongomin, afisa mkuu katika moja ya kampuni za kamari za Uganda, anasema kampuni za kamari hazipaswi kulaumiwa kwa vurugu za soka.

"Watu hawana ujuzi wa kudhibiti matarajio yao na hasira," ameiambia BBC, akibainisha juhudi za makampuni kuhimiza kucheza kamari kwa ustaarabu.

Kuna zaidi ya maduka 2,000 ya kamari kote Uganda, hilo pia huleta faida kubwa kwa serikali, ambayo ilikusanya takribani dola za kimarekani milioni 50 (£40m) katika mapato ya kodi kutokana na kamari mwaka jana, kulingana na vyombo vya habari vya ndani.

Umri, Umasikini na Pombe

Baadhi wanasema ushabiki wa uadui upo zaidi kwa mashabiki wa Arsenal na Man Utd wa Uganda. Wanasema hilo linatokana na umri na historia.

Linika, mfuasi wa Liverpool, anasema timu yake ina mashabiki wengi wazee na wale ambao wana kipato kizuri. Huku mashabiki wa Arsenal na Man Utd wakitoka katika maeneo maskini zaidi.

"Kwa sasa tuko juu ya jedwali la Ligi Kuu ya England, na ni nadra kusikia shabiki wa Liverpool aliyehusika katika vurugu," anasema.

Pamela Icumar, maarufu kama Mama Liverpool kwa sababu ya kujitolea sana kwa Reds, na sehemu ya klabu ya mashabiki wa kike pekee huko Kampala, anasema mashabiki wenzake wanajua jinsi ya kudhibiti hisia zao "hata tunapopoteza".

Lakini shabiki wa Arsenal, Agnes Katende, ameikaa hoja hii, nilipokutana naye Kampala.

Kwa Solomon Kutesa, katibu wa Klabu rasmi ya Wafuasi wa Arsenal nchini Uganda, utamaduni wa unywaji pombe nchini humo ndio wa kulaumiwa kwa vurugu za soka.

"Baadhi ya mashabiki hutazama michezo wakiwa wamelewa na inakuwa vigumu kuwazuia timu zao zinaposhindwa," ameiambia BBC.

Wengine wanapendekeza kuwapeleka mashabiki katika viwanja vya michezo na kuwatoa baa. Wanaamini hilo linaweza kupunguza hali hiyo na kufufua ligi kuu ya Uganda.

Kufufua soka la ndani

"Kizazi cha sasa kinajua soka la Ulaya pekee. Ikiwa tutawekeza zaidi kwenye ligi ya ndani tunaweza kufanikiwa kuondoa umakini mkubwa kwa michezo ya nje," anasema Bw Kyambadde, huku akikiri kwamba ligi ya ndani ina sifa mbaya na ukosefu wa wachezaji nyota.

Mwanasoka wa zamani Tom Lwanga, ambaye aliichezea timu ya taifa ya Uganda, ilipotinga fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika la 1978, anakubali hilo.

"Tulijizolea umaarufu kwa sababu tulikuwa tukicheza wakati viwanja vimejaa. Tunahitaji kurejea enzi hizo na kudhibiti shamrashamra za soka la Ulaya," aliniambia katika kiwanja kitupu cha Phillip Omondi mjini Kampala tulipokuwa tukitazama mechi ya mpira.

Wengine wanalaumu ukosefu wa matangazo ya moja kwa moja ya televisheni kwa kuzorota ligi ya Uganda.

Asuman Basalirwa, mwenyekiti wa Klabu ya Bunge la Uganda, ambaye pia alikuwa katika uwanja wa Omondi, ni miongoni mwa wale wanaojaribu kuimarisha soka la ndani.

"Mimi ni miongoni mwa wabunge wachache wanaotazama soka la ndani na tunataka kuona viongozi wengi zaidi hata rais wakija viwanjani kusaidia timu za ndani," anasema.

Lakini kwa Bw Kutesa, ambaye mapenzi yake kwa Arsenal yalianza tangu enzi za wachezaji kama Nwankwo Kanu na Thierry Henry, timu ya Arsenal ni muhimu kwake.


Makala Zinazohusiana


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved