Achraf Hakimi apigwa busu na mamake baada ya kufunga penalti ya ushindi (+video)

Hakimi alipiga penalti ya maamuzi na kuipa Morocco ushindi.

Muhtasari

•Mamake Hakimi alirekodiwa akimbusu kwenye shavu la kulia, karibu na mdomo kwa kujivunia mafanikio ya mwanae

•Morocco sasa itamenyana na Ureno katika hatua ya raundi ya robo fainali mnamo Jumamosi, Desemba 10.

apigwa busu na mamake baada ya kupata ushindi dhidi ya Uhispania.
Beki wa Morocco Achraf Hakimi apigwa busu na mamake baada ya kupata ushindi dhidi ya Uhispania.
Image: HISANI

Morocco imekuwa taifa la nne la Afrika kufuzu kwa robo fainali ya Kombe la Dunia baada ya kuishinda Uhispania 3-0 katika mikwaju ya penalti.

Mchuano wa kusisimua kati ya Morocco na mabingwa hao wa Kombe la Dunia mwaka wa 2010 haukuwa na bao lolote katika muda wa kawaida na muda wa ziada na hivyo ikabidi kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti.

Kiungo wa kati wa Sampdoria Abdelhamid Sabiri alikuwa wa kwanza kuchukua jukumu la taifa na bara zima la Afrika ambalo lilikuwa nyuma ya Morocco na bila tatizo akapiga mpira kumpita kipa wa Uhispania Unai Simon. Hii ni kabla ya mkwaju wa penalti wa  kiungo wa Uhispania Pablo Sarabia kugonga mtamba panya.

Mshambulizi  wa Morocco Hakim Ziyech alifanikiwa kufunga mkwaju wake wa penalti huku juhudi za Carlos Soler na Sergio Busquets zikanguka kwenye mikono ya mlinda lango wa Morocco Yassine Bounou.

Beki wa kulia wa PSG Achraf Hakimi alipiga penalti ya maamuzi na kuipa Morocco ushindi. Baada ya kufunga penalti hiyo Hakimi alisherehekea huku akielekea kwa mama yake ambaye alikuwa akitazama mechi hiyo.

Mamake Hakimi alirekodiwa akimbusu kwenye shavu la kulia, karibu na mdomo kwa kujivunia mafanikio ya mwanae. Beki huyo alizaliwa Madrid, Uhispania kwa wazazi wa Morocco ambao walikuwa wamehamia nchi hiyo ya Ulaya kwa ajili ya kazi.

Hapo awali Hakimi aliwahi kufunguka kuhusu jinsi wazazi wake walihangaika nchini Uhispania ili kuhakikisha amefaulu.

"Mama yangu alisafisha nyumba na baba alikuwa mfanyibiashara wa mtaani, tunatoka katika familia ya kawaida ambayo ilihangaika kutafuta riziki, leo napambana kila siku kwa ajili yao, walijitoa mhanga kwa ajili yangu, waliwanyima ndugu zangu mambo mengi kwa ajili yangu. kufanikiwa," alisema mwaka wa 2018.

Morocco sasa itamenyana na Ureno katika hatua ya raundi ya robo fainali mnamo Jumamosi, Desemba 10.