Africa Football League: Esperance Tunis, Wydad waungana na Sundowns, Al Ahly katika nusu fainali

Mechi za nusu fainali zitachezwa mnamo Oktoba 29 na Novemba 1.

Muhtasari

•Esperance Tunis ya Tunisia na Wydad ya Morocco walifuzu kwa nusu fainali baada ya kuzibwaga TP Mazembe ya Kongo na Enyimba ya Nigeria.

• Wydad na Esperance Tunis wanaungana na Al Ahly na Mamelodi Sundowns  katika orodha ya klabu ambazo zimefuzu kwa nusu fainali.

Wydad waliwapiga Enyimba kufuzu kwa nusu fainali.
Image: AFL

Michuano miwili ya mwisho ya robo fainali ya Ligi ya Soka ya Afrika (AFL) ilikamilika siku ya Alhamisi jioni.

Vigogo wawili wa Afrika Kaskazini, Esperance Tunis ya Tunisia na Wydad ya Morocco walifuzu kwa nusu fainali baada ya kuzibwaga TP Mazembe ya Kongo na Enyimba ya Nigeria mfululizo.

Esperance Tunis ilishinda dhidi ya TP Mazember kwa jumla ya mabao 3-1 baada ya kuwalaza 3-0 kwenye uwanja wa Stafe Olympique Hammadi Agrebi siku ya Alhamisi, mwendo wa saa kumi na mbili asubuhi. TP Mazembe ilishinda 1-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Stade TP Mazembe mjini Lubumbashi, Kongo mnamo Oktoba 22.

Wydad pia ilishinda 3-0 dhidi ya Enyimba kwenye Uwanja wa Stade Mohamed V mjini Casablanca, Morocco Alhamisi usiku na kufanya matokeo ya mwisho kuwa 4-0. Miamba hao wa Morocco walikuwa wameshinda 0-1 wakiwa ugenini dhidi ya klabu hiyo ya Nigeria katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio mjini Uyo, Nigeria Oktoba 22.

Wydad na Esperance Tunis sasa wanaungana na Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika orodha ya klabu ambazo zimefuzu kwa nusu fainali ya shindano hilo jipya la Afrika.

Mamelodi na Al Ahly zitamenyana kuwania kufuzu kwa fainali katika uwanja wa Loftus Verfeld mjini Pretoria, Afrika Kusini Oktoba 29 kabla ya kukutana kwa mkondo wa pili nchini Misri mnamo Novemba 1.

Wydad itawakaribisha Esperance Tunis  kwa mechi ya mkondo wa kwanza Oktoba 29 katika Uwanja wa Stade Mohamed V mjini Casablanca, Morocco kabla ya kukutana kwa mkondo wa pili katika Uwanja wa Stade Olympique Hammadi Agrebi mjini Rades, Tunisia mnamo Novemba 1.