Al Hilal yataka kumnunua Kylian Mbappe bilioni 47.2, kumlipa bilioni 9.2 kila mwezi

Al Hilal wanaripotiwa kuwa tayari kumlipa bilioni 9.2 kwa mwezi.

Muhtasari

•Al Hilal imewasilisha dau la rekodi la shilingi bilioni 47.2 kwa PSG kumnunua mshambuliaji wa Ufaransa Kylian Mbappe.

•Mkataba wa Mbappe na PSG unatarajiwa kumalizika mwezi Juni mwaka ujao na anaonekana kukataa kabisa kusaini mkataba mpya.

Image: Instagram

Klabu ya Saudi Arabia, Al Hilal imewasilisha dau la rekodi la pauni milioni 259 (Ksh 47.2B) kwa Paris Saint Germain (PSG) kumnunua mshambuliaji wa Ufaransa Kylian Mbappe.

Miamba hao wa soka wa Ufaransa ambao hawajakuwa katika uhusiano mzuri na mshambuliaji huyo imeripotiwa kukubali ombi hilo la kuvutia na kukubali kumuuza.

Hata hivyo, Al Hilal bado haijaanza mazungumzo na Mbappe mwenyewe kama ripoti kutoka Ulaya zinavyoonyesha. Iwapo nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa atakubali uhamisho huo, basi atakuwa mchezaji ghali zaidi wa soka wa wakati wote.

Klabu hiyo ya Saudia imeripotiwa kuandaa ofa nzuri ya mshahara kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 huku wakisemekana kuwa tayari kumlipa bilioni 9.2 kwa mwezi. Hii ni kumaanisha mchezaji huyo atakuwa anapokea mshahara wa takriban shilingi milioni 30.7 kwa siku, milioni 1.3 kwa saa na Ksh 53,241 kwa dakika moja.

Mbappe anadaiwa kutovutiwa na uhamisho wa kuenda Saudia na anasemekana kupendelea kusalia PSG hadi mwisho wa 2023/24 atakapojiunga na Real Madrid. Ripoti kutoka Ulaya zinaonyesha kuwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 tayari ameshaafikia makubaliano na miamba hao wa soka wa Uhispania.

Mkataba wa Mbappe na PSG unatarajiwa kumalizika mwezi Juni mwaka ujao na anaonekana kukataa kabisa kusaini mkataba mpya. PSG inaripotiwa kutokuwa tayari kumpoteza mshambuliaji huyo mahiri bure na ndiyo maana wanajaribu kumuuza.