Arsenal na Man City vitani kushindania saini ya Declan Rice

Rice yuko tayari kujiunga na moja ya klabu hizo ambayo itawasilisha ofa itakayokubalika.

Muhtasari

•City wanajipanga kuwasilisha ombi lao la ufunguzi la nahodha huyo wa West Ham mwenye umri wa miaka 24.

•West Ham wanataka angalau pauni milioni 100 ili kumwachilia mchezaji huyo wa Uingereza kuondoka.

Image: TWITTER// DECLAN RICE

Klabu ya Manchester City imejitosa katika pambano la kupata saini ya kiungo wa West Ham na timu ya taifa ya Uingereza, Declan Rice.

Duru za kuaminika zinasema washindi hao wa vikombe vya EPL, Champions League na FA mwaka wa 2023 wanajipanga kuwasilisha ombi lao la ufunguzi la nahodha huyo wa West Ham mwenye umri wa miaka 24.

Inaripotiwa kuwa City tayari imeshaulizia kwa klabu hiyo ya London na mchezaji mwenyewe kuhusu hali yake na upatikanaji wake. Rice yuko tayari kujiunga na moja ya klabu hizo ambayo itawasilisha ofa itakayokubalika.

Klabu hiyo inayoongozwa na Pep Guardiola inaripotiwa kumtamani sana kiungo huyo wa kati na ombi kubwa linatarajiwa kuwasilishwa hivi karibuni ili kukabiliana na Arsenal katika mbio za kujizolea saini ya mchezaji huyo

Wanabunduki tayari wametoa ofa mbili kwa Rice ila West Ham wamezitupilia mbali baada ya kutofikia matakwa yao. Ofa ya pili ya pauni milioni 90 (Ksh 16.1bilioni) ilikataliwa siku ya Jumanne ila klabu hiyo ya London Kaskazini bado haijakufa moyo katika kupambania saini ya mchezaji huyo.

West Ham wanataka angalau pauni milioni 100 ili kumwachilia mchezaji huyo wa Uingereza kuondoka.

Arsenal inaripotiwa kummezea mate sana Rice na wana matumaini ya kumsajili ili aweze kujaza nafasi ya Thomas Partey na Granit Xhaka ambao wanatarajiwa kuondoka kabla ya msimu wa EPL 2023/24 kung'oa nanga.