Aubameyang atamani kurejea katika klabu yake ya zamani kufuatia msimu mbaya Chelsea

Auba ameweka wazi hana mpango wa kusalia Stamford Bridge baada ya msimu wa 2022/23 kukamilika.

Muhtasari

•Auba amedokeza nia ya kusitisha mkataba wake na Chelsea huku akishiria nia ya kurejea katika klabu hiyo ya Barcelona. 

•"Ningependa kurejea Barcelona lakini tutaona," alisema Aubameyang katika mahojiano na Djam Life.

Mshambuliaji wa Chelsea Pierre-Emerick Aubameyang
Image: HISANI

Ni wazi kuwa mshambulizi wa Gabon, Pierre-Emerick Aubameyang hana mpango wa kusalia Stamford Bridge baada ya msimu wa 2022/23 kukamilika.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 33 amedokeza nia ya kusitisha mkataba wake na Chelsea huku akishiria nia ya kurejea katika klabu hiyo ya Barcelona. Aubameyang alitia saini mkataba wa miaka miwili na The Blues baada ya kujiunga nao mnamo mwezi Septemba mwaka jana kwa uhamisho wa £10m kutoka Barcelona.

Kufuatia msimu mbaya katika klabu hiyo yenye maskani yake jijini London, nahodha huyo wa zamani wa Arsenal sasa anatazamia kuondoka Stamford Bridge mwishoni mwa msimu huu na kujaribu kufufua mchezo wake kwingineko, huku Chelsea  pia wakiashiria furaha ya kukatiza uhusiano naye.

"Ningependa kurejea Barcelona lakini tutaona," alisema Aubameyang katika mahojiano na Djam Life.

Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 33 amekuwa na kipindi kigumu katika Chelsea, akiwa amefunga mabao matatu pekee katika mechi 21. Ameachwa nje ya kikosi cha washindi wa Ligi ya Mabingwa mwaka wa 2021 mara kadhaa.

Alipoulizwa kuhusu klabu gani angependa kujiunga nayo baadaye, alisema “Sijui. Tutaona. Naipenda Barca.

Aubameyang aliondoka Barcelona Septemba mwaka jana na kujiunga na Chelsea baada ya kuchezea klabu hiyo ya Uhispania kwa miezi kadhaa. Aliondoka Arsenal Januari 2022 kama mchezaji huru baada ya mkataba wake na klabu hiyo kusitishwa kufuatia uhusiano mbaya na kocha Mikel Arteta.