Beki Recce James avunja kimya baada ya kuteuliwa kuwa nahodha mpya wa Chelsea

James alitoa ahadi kubwa kwa mashabiki wa Chelsea kwamba yuko tayari kujitolea kuiongoza klabu hiyo kutwaa mataji.

Muhtasari

•Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alitoa shukrani kwa wote ambao wamemuunga mkono katika taaluma yake ya soka.

•The Blues walimtangaza beki huyo wa kulia kama nahodha wao mpya baada ya kuondoka kwa Mhispania César Azpilicueta.

ameteuliwa kuwa nahodha mpya wa Chelsea.
Recce James ameteuliwa kuwa nahodha mpya wa Chelsea.
Image: TWITTER// CHELSEA

Beki wa Uingereza Recce James amesema kufanywa nahodha mpya wa klabu ya Chelsea ni heshima kubwa na jambo la kujivunia kwake na kwa familia yake.

Katika taarifa yake Jumatano jioni, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 alitoa shukrani kwa wote ambao wamemuunga mkono katika taaluma yake ya soka.

James wakati huo huo alitoa ahadi kubwa kwa mashabiki wa Chelsea kwamba yuko tayari kujitolea kuiongoza klabu hiyo kutwaa mataji.

"Nahodha wa Chelsea. Ni wakati wa heshima na fahari kwangu na familia yangu. Kutoka chini ya moyo wangu nataka kuwashukuru wote waliosaidia katika safari.

Jukumu hili ni geni kwangu lakini nitafanya kila kitu ili kuiongoza klabu yetu kurudi tunapohitaji kuwa. Kushinda mataji. Tuonane Stamford Bridge,” James alisema katika taarifa yake.

Siku ya Jumatano, The Blues walimtangaza beki huyo wa kulia kama nahodha wao mpya baada ya kuondoka kwa Mhispania César Azpilicueta. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 aliondoka Stamford Bridge mwezi uliopita na kujiunga na klabu ya soka ya Atletico Madrid iliyo nyumbani kwao Uhispania.

"Reece James amethibitishwa rasmi kuwa nahodha mpya wa Klabu ya Soka ya Chelsea," ilisoma taarifa ya Chelsea Jumatano jioni.

Kocha mkuu Mauricio Pochettino alijawa na sifa tele kwa mchezaji huyo wa kimataifa wa nchi ya Uingereza mwenye umri wa miaka 24 ambaye ameichezea klabu hiyo tangu 2018.

Katika ujumbe wake, Pochettino alisisitiza kuwa anajivunia uamuzi wake huo na kusema kwamba anafurahishwa na James kuongoza klabu hiyo msimu ujao.

"Anaongoza kwa mfano na mtazamo wake na kujitolea kwake kwa Chelsea imekuwa wazi katika kipindi chote cha maandalizi ya msimu mpya. Alijivunia wadhifa huo wakati wa ziara yetu ya kiangazi na atachukua changamoto ya kukiongoza kikosi chetu kwa mbinu na mawazo yake,” Pochettino alisema.

Recce James alijiunga na akademi ya soka ya Chelsea akiwa na umri mdogo sana na alitia saini mkataba wake wa kwanza na klabu hiyo mwaka wa 2018 kabla ya kwenda kwa mkopo katika klabu ya Championship ya Wigan Athletic.