Chelsea wamkaribisha Enzo Fernandez kwa wimbo mzuri baada ya kutua London

Fernandez sasa ndiye mchezaji ghali zaidi duniani.

Muhtasari

•The Blues walimtambulisha kiungo huyo kama mchezaji wao mpya Jumatano jioni baada ya kuwasili kutoka Ureno.

•Fernandez alitia saini mkataba wa miaka minane unusu hadi 2031 na atavalia jezi nambari 5.

Enzo Fernandez
Image: TWITTER// CHELSEA

Kiungo wa kati Enzo Fernandez hatimaye yuko jijini London, Uingereza baada ya kukamilisha uhamisho wake kutoka Benfica kwenda Chelsea.

Stamford Bridge sasa itakuwa makao mapya kwa mshindi huyo wa Kombe la Dunia la 2022 mwenye umri wa miaka 22 kwa miaka minane na nusu ijayo baada ya kukamilisha taratibu za uhamisho siku ya Jumatano.

The Blues walimtambulisha kiungo huyo kama mchezaji wao mpya Jumatano jioni baada ya kuwasili kutoka Ureno.

"Bingwa wa dunia katika Bluu ya Chelsea," waliandika chini ya picha ya mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Argentina.

Klabu hiyo ya London pia ilitengeneza wimbo mtamu wa kumkaribisha Fernandez katika makao yake mapya.

"Hii ni La T y La M kwa Enzo. Kutoka Argentina hadi Uingereza, na tabasamu la mtu ambaye alishinda taji la tatu, bingwa wa dunia, tayari unajua ni nani: Enzo Fernandez, anafika London," wimbo huo ulisema.

Fernandez sasa ndiye mchezaji ghali zaidi duniani baada ya Chelsea kugharamika pauni milioni 107 kumsajili kutoka Benfica. Alivunja rekodi ambayo ilikuwa imeshikiliwa na mshambulizi wa Uingereza, Jack Grealish ambaye alisajiliwa na Manchester City kutoka Aston Villa kwa pauni milioni 100 mwaka wa 2021.

Kiungo huyo mahiri ambaye alichaguliwa kama Mchezaji Bora Chipukizi katika Kombe la Dunia la FIFA la 2022 nchini Qatar alitia saini mkataba wa miaka minane unusu hadi 2031 na atavalia jezi nambari 5.