Christiano Ronaldo acheka Messi kutunukiwa tuzo ya Ballon d'Or 2023

Christiano ni miongoni mwa watu waliopenda chapisho la mwanahabari akikejeli tuzo za Ballon d'Or 2023.

Muhtasari

•Mshambulizi Christiano Ronaldo ameonekana kucheka hatua ya kumtunuku mpinzani wake mkubwa, Lionel Messi taji la Ballon d’Or.

•Rancero alidai kuwa Messi hakustahili hata tuzo nyingine tatu za Ballon d’Or ambazo alipewa siku za nyuma.

Messi na Ronaldo.
Messi na Ronaldo.
Image: Facebook

MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Al Nassr FC, Christiano Ronaldo ameonekana kucheka hatua ya kumtunuku mpinzani wake mkubwa, Lionel Messi taji la Ballon d’Or.

Baada ya nahodha huyo wa timu ya soka ya Argentina kutunukiwa tuzo hiyo ya kifahari mjini Paris, Ufaransa usiku wa Jumatatu, kundi la mashabiki na wataalamu wa soka wamejitokeza kukosoa hatua hiyo na wengine hata kudai kuwa mchezaji mwingine alistahili tuzo hiyo.

Mmoja wa watu waliojitokeza kuelezea kusikitishwa kwao na tuzo ya Ballon d'Or za mwaka huu ni mwandishi wa habari za michezo maarufu wa Uhispania, Tomás Roncero ambaye alidai kuwa kulikuwa na upendeleo mkubwa na kwamba Messi hakustahili tuzo hiyo.

"Vipi marafiki. Tulichojua kimetokea. Walikuwa wanakwenda kumpa Ballon d'Or nyingine Messi.  Alienda kustaafu Miami, lakini tayari alikuwa anaonekana amestaafu PSG kuelekea maandalizi ya Kombe la Dunia. Alishinda Kombe la Dunia. , ndio, lakini kwa penalti 6 kwa niaba yao,” Roncero aliwaambia waandishi wa habari Jumatatu usiku.

Aliendelea kudai kuwa staa huyo wa Inter Miami mwenye umri wa miaka 36 hakustahili hata tuzo nyingine tatu za Ballon d’Or ambazo alipewa siku za nyuma.

"Kombe la Dunia lilikuwa miezi 10 iliyopita, tuko Novemba. Messi ana Ballon d'Or nane vizuri, anapaswa kuwa na tano, ana Ballon d'Ors ya [Andres] Iniesta na Xavi, [Robert] Lewandowski ambaye alishinda mataji sita katika msimu mmoja na Haaland ambaye alikuwa mfungaji bora wa kila kitu, " alisema.

Ukurasa maarufu wa habari wa michezo uliweka video ya Bw Roncero akizungumza na cha kushangaza, Christiano Ronaldo ni miongoni mwa watu waliopenda chapisho hilo na kutoa maoni.

Katika jibu lake la emoji, staa huyo wa soka mwenye umri wa miaka 38 alionekana kukubaliana na maoni ya Roncero na kukejeli kutunukiwa kwa mpinzani wake, Messi.

"😂😂😂😂," Ronaldo aliandika.

Image: INSTAGRAM

Hafla ya 67 ya Ballon d’Or ilifanyika usiku wa Jumatatu, Oktoba 30 kwenye ukumbi wa Théâtre du Châtelet jijini Paris, Ufaransa ambapo kulikuwa na washindi tofauti katika vipengele mbalimbali.

Lionel Messi alishinda taji la Ballon d’Or kwa Wanaume kwa mara ya nane katika maisha yake ya soka baada ya kupata mafanikio makubwa katika mwaka mmoja uliopita. Mshambuliaji huyo matata mwenye umri wa miaka 36 hapo awali aliwahi kushinda tuzo hiyo mwaka wa 2009, 2010, 2011, 2012, 2015, 2019 na 2021.

Erling Haaland wa Man City na Norway aliibuka wa pili huku staa wa PSG na Ufaransa, Kylian Mbappe akishika nafasi ya tatu.

Wengine walioingia kwenye orodha ya kumi bora ni Rodri wa Manchester City, Vinicius Junior wa Real Madrid, Julian Alvarez wa Manchester City, Victor Osimhen wa Napoli, Bernardo Silva wa Manchester City na Luka Modric wa Real Madrid.