Christiano Ronaldo afichua mipango yake ijayo baada ya mwisho wa msimu wa 2022/23

Mreno huyo amefichua kuwa nia yake ni kubaki katika klabu yake ya sasa ya Al Nassr.

Muhtasari

•Ronaldo aliweka wazi kuwa ana furaha katika klabu hiyo ya nchi ya Saudi Arabia na anatamani kuendelea kutoa huduma zake pale.

•Ronaldo alizungumzia vizuri tetesi za mwenzake wa zamani katika Real Madrid, Karim Benzema kujiunga na ligi hiyo.

Image: TWITTER// CHRISTIANO RONALDO

Mchezaji wa Kimataifa wa Ureno Christiano Ronaldo amefichua kuwa nia yake ni kubaki katika klabu yake ya sasa ya Al Nassr.

Akizungumza katika mahojiano, mshambuliaji huyo matata mwenye umri wa miaka 38 aliweka wazi kuwa ana furaha katika klabu hiyo ya nchi ya Saudi Arabia na hivyo anatamani kuendelea kutoa huduma zake pale.

"Nina furaha na ninataka kuendelea na nitaendelea hapa. Msimu ujao timu itakuwa bora zaidi. Tumeimarika katika kipindi cha miezi mitano au sita  iliyopita, na nina imani kuwa tutashinda mataji hivi karibuni." Ronaldo aliambia SPL Chat.

Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United alisifia ligi ya Saudi Arabi na kubainisha kuwa ina nafasi ya kukua zaidi.

"Nadhani ligi hii ni nzuri sana lakini nadhani tuna nafasi nyingi sana za kukua. Nadhani ligi ni nzuri, na ina ushindani. Tuna timu nzuri sana, tuna wachezaji wazuri sana wa kiarabu," Ronaldo alisema.

Huku akizungumza kuhusu marekebisho ambayo angependekeza kufanyika, mshambuliaji huyo alisema, "Miundombinu nadhani wanahitaji kuboresha kidogo zaidi. Waamuzi na mfumo wa VAR pia. Nafikiri wanapaswa kuwa wepesi zaidi. Nadhani mambo mengine madogo wanahitaji lakini nina furaha hapa."

Ronaldo pia alizungumzia vizuri tetesi za mwenzake wa zamani katika klabu ya Real Madrid, Karim Benzema na mastaa wengine kujiunga na ligi hiyo.

"Wanakaribishwa, ligi itaimarika, na kwa sasa ina wazuri wa kigeni na Waarabu," alisema.

Ronaldo alijiunga na Al Nassr baada ya kuaga Man United mwezi Januari kufuatia mahojiano yake yenye utata na mtangazaji wa Uingereza, Piers Morgan ambapo alifichua mambo ya ndani ya klabu hiyo hadharani.

Akizungumza kwenye mahojiano nchini Ureno, kabla ya mechi zao za kipindi cha mapumziko ya kimataifa, mshambulizi huyo alikiri kwamba alikuwa na kipindi kibaya cha taaluma yake ya soka wakati akiwa katika United.

"Wakati mwingine, lazima upitie mambo mengine ili kuona ni nani aliye upande wako. Sina shida kusema, nilikuwa na kipindi kibaya, lakini hakuna wakati wa majuto," alisema.

Kipindi hicho, mshambulizi huyo wa  Ureno alibainisha kuwa taaluma yake ya soka inaendelea vizuri kwa sasa na kusema kuwa kipindi chake kibaya katika Manchester United kilikuwa sehemu ya ukuaji wake.