EFL Cup: Usiku wa machozi kwa vilabu vya London

Arsenal, Chelsea na Tottenham hawatasonga mbele hadi hatua ifuatayo ya kombe hilo.

Muhtasari

•Arsenal, Chelsea, Tottenham zilipata kichapo kutoka kwa washindani wao katika mechi za ufunguzi za EFL Carabao cup.

•Kupoteza huko kunamaanisha mwisho wa safari ya Kombe la EFL kwa vilabu hivyo vitatu vya London.

Image: TWITTER// CHELSEA

Usiku wa Jumatano ulikuwa usiku mbaya wa kusahaulika kwa vilabu vikuu vya Premier League kutoka jiji la London.

Arsenal, Chelsea na Tottenham ambazo zote zinaorodheshwa miongoni mwa vilabu sita bora kwenye Ligi Kuu ya Uingereza zilipata kichapo kutoka kwa washindani wao katika mechi za ufunguzi za EFL Carabao cup.

Wanabunduki ambao walikuwa wakicheza nyumbani Emirates walipoteza 1-3 dhidi ya Brighton & Hove Albion. Mabao ya Danny Welbeck (Penalti), Kaoru Mitoma na Tariq Lamptey yalitosha kuwazima vijana wa Mikel Arteta ambao wanaendelea kutesa kwenye EPL huku bao la pekee la Eddie Nketiah likiwafuta machozi.

Vijana wa Pep Guardiola waliwika nyumbani Etihad dhidi ya Chelsea na kuwazima kwa mawili bila jawabu. Riyad Mahrez na Julian Alvarez walifanikisha ushindi huo na kuwezesha City kuendelea hadi ngazi inayofuata ya shindano hilo huku The Blues wakiungana na majirani wao Arsenal kurudi nyumbani na huzuni.

Tottenham vilevile hawakuwa na bahati katika mechi yao dhidi ya Nottingham Forest. Klabu hiyo ambayo inavuta mkia kwenye Premier League iliweza kuwika kwenye Carabao kwa kuzoa ushindi wa 2-0 dhidi ya vijana wa Antonio Conte.

Kupoteza huko kunamaanisha mwisho wa safari ya Kombe la EFL kwa vilabu hivyo vitatu vya London. Arsenal, Chelsea na Tottenham sasa hawatasonga mbele hadi hatua ifuatayo ya kombe hilo.

Mancity sasa watatafuta kusonga mbele zaidi na kutwaa tena kombe hilo ambalo walishinda msimu 2020/21.