Fahamu kwa nini wachezaji katika ligi za Ulaya wanapanga kufanya mgomo hivi karibuni

Katika siku za hivi majuzi, kumekuwa na mazungumzo mengi kuhusu uwezekano wa kugoma kwa wachezaji.

Muhtasari

•Rodri aliomba kuzingatiwa kupunguzwa kwa mechi, na sasa beki wa Barcelona Jules Kounde pia amezungumza kuhusu suala hilo.

•Rodri alidokeza kuhusu uwezekano wa wachezaji kugoma hivi karibuni akibainisha kuwa hawana chaguo lingine kwa sasa.

usio na watu
Uwanja wa Etihad usio na watu
Image: HISANI

Wachezaji katika ligi kuu za soka katika bara Ulaya wameendelea kulalamika kuhusu kuongezeka kwa idadi ya mechi katika msimu mmoja wa soka.

Katika siku za hivi majuzi, kumekuwa na mazungumzo mengi kuhusu uwezekano wa kugoma kwa wachezaji, mazungumzo ambayo yameletwa na suala hilo ambalo linatishia utimamu wa wachezaji.

Staa wa Manchester City na Uhispania Rodri Hernandez aliomba kuzingatiwa kupunguzwa kwa mechi mapema wiki hii, na sasa beki wa Barcelona Jules Kounde pia amezungumza kuhusu suala hilo.

Akizungumza kabla ya mechi ya ufunguzi ya Ligi ya Mabingwa ya Barcelona dhidi ya Monaco, Kounde alikiri kwamba atakuwa tayari kwa wazo la kugoma kutaka wachezaji wasikilizwe. Alibainisha kuwa wachezaji wamekuwa wakilalamika kwa muda sasa lakini kelele zao zinaonekana kuangukia maskio yaliyotiwa pamba, sababu ya wao kupendekeza kugoma.

“Nakubaliana na Rodri. Kila mwaka tuna mechi nyingi na kupumzika kidogo. Tumekuwa tukisema hivi kwa miaka 3-4 na hakuna anayesikiliza wachezaji… Wakati utafika ambapo tutalazimika kugoma ili kusikilizwa na wale wanaoamua,” Kounde alisema.

Aliongeza, "Tunachukulia hatari inayoongezeka na unaweza kuona kuwa kuna majeraha zaidi kwa sababu kuna muda mdogo wa kupumzika. Wale wanaocheza Kombe la Dunia la Vilabu watafikisha takriban michezo sabini kwa msimu, jambo ambalo ni wazimu.”

Kiungo wa kati wa Manchester City na mteule wa tuzo ya Ballon d'Or Rodri amekuwa mmoja wa wachezaji wenye sauti kubwa kuhusiana na suala la uwezekano wa wanasoka kugoma kutokana na ratiba iliyojaa ambayo inaonekana kuongezeka kila msimu unaopita.

Mapema wiki hii, alidokeza kuhusu uwezekano wa wachezaji kugoma hivi karibuni akibainisha kuwa hawana chaguo lingine kwa sasa.

"Nadhani tunakaribia hilo [kugoma. Ni maoni ya jumla ya wachezaji, na kama itaendelea hivi, hatutakuwa na chaguo lingine. Nafikiri ni jambo ambalo linatutia wasiwasi. Sisi ndio watu wanaoteseka,” Rodri alisema katika mkutano na wanahabari mapema wiki hii.

Kiungo huyo mahiri alibainisha kuwa sehemu mwafaka ambayo mchezaji anaweza kucheza kwa kiwango cha juu ni kati ya mechi 40 na 50 kwa msimu.

"Baada ya hapo, unashuka kwa sababu haiwezekani kuendeleza kiwango cha kimwili. Mwaka huu, tutaenda hadi 70, labda [mechi] 80, [inategemea] jinsi unavyoenda kwenye mashindano. Nadhani ni nyingi sana. 

Tunapaswa kujitunza wenyewe, kwa sababu sisi ni wahusika wakuu wa mchezo huu au biashara. Sio kila kitu ni pesa au uuzaji, pia ni ubora wa shoo. Ninapopumzika, nisipochoka, ninafanya vizuri zaidi. Na kama watu wanataka kuona soka bora, tunahitaji kupumzika," Rodri alisema.