Firmino avunja kimywa baada ya kuachwa nje ya kikosi cha Brazil

Mshambulizi huyo amekiri kwamba hakutarajia kuachwa nje ya kikosi hicho.

Muhtasari

•Mshambulizi matata wa Liverpool Roberto Firmino aliachwa nje ya kikosi cha Brazil, jambo ambalo lilizua gumzo kubwa.

•Aidha aliwashukuru wote ambao walimtumia jumbe za kumpa moyo baada ya kachwa nje ya kikosi hicho.

Image: INSTAGRAM// ROBERTO FIRMINO

Siku ya Jumatatu, Kocha wa Brazil Adenor Leonardo Bacchi almaarufu Tite alitaja kikosi kitakachoambatana naye kwenye Mashindano ya Kombe la Dunia yatakayofanyika nchini Qatar siku chache zijazo.

Tite alitaja kikosi cha wachezaji 26 ambacho kilijumuisha washambulizi Gabriel Jesus na Gabriel Martinelli wa Arsenal , Richarlison wa Tottenham na Antony wa Manchester United, lakini mshambulizi matata wa Liverpool Roberto Firmino akaachwa nje, jambo ambalo lilizua gumzo kubwa.

Mshambulizi huyo jezi nambari 9 wa The Reds amekiri kwamba hakutarajia kuachwa nje ya kikosi hicho na kufichua kuwa ilikuwa ndoto yake kuiwakilisha nchi yake katika michuano hiyo ya kimataifa.

Firmino hata hivyo aliweka wazi kuwa yuko sawa na maamuzi ya kocha Tite na kudokeza kuwa kuna nyakati zingine nyingi za awali za kujivunia ambazo amewakilisha taifa lake  kwenye ulingo wa kidunia.

"Kombe la Dunia ni ndoto kwa kila mchezaji na kwangu haitakuwa tofauti. Jana (Jumatatu) mambo hayakwenda jinsi nilivyowazia au kutamani katika maisha yangu lakini naweza kutazama nyuma na kuwa na moyo wa shukrani kwa Mungu kwamba tayari ameniruhusu kuishi ndoto hiyo pamoja na zingine nyingi," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Aidha aliwashukuru wote ambao walimtumia jumbe za kumpa moyo baada ya kachwa nje ya kikosi hicho.

Pia aliwapongeza na kuwatakia mafanikio wachezaji wenzake waliochaguliwa kuwakilisha nchi yao.

"Nachukua fursa hii kutoa heshima yangu na kuwapongeza wote ambao waliitwa. Ilikuwa, ni, na daima itakuwa heshima kutetea nchi yangu hasa kwa zawadi ambayo Bwana alinipa. Ninakaa hapa nikiwa na hakika kuwa Mungu ana mipango bora kwangu na nikitumai kwamba wakati wangu unakuja,"

Firmino alitumia mistari ya Biblia ya Yeremia 29:11 na Isaya 23:6  kueleza hisia zake kuhusu suala zima la kuachwa nje..

"Kwa maana ninajua mipango niliyo nayo kwa ajili yenu,’  anasema Yehova, ‘mipango ya kuwafanikisha na si ya kuwadhuru ninyi, mipango ya kuwapa nyinyi matumaini ya siku za usoni'" alisema.