Gor Mahia waibuka mabingwa wa ligi ya Kenya kwa mara ya 20

Klabu hiyo sasa ndiyo timu yenye mafanikio zaidi nchini.

Muhtasari

• Gor Mahia waliibuka mabingwa mara 20 wa ligi kuu nchini FKFPL baada ya kuwalaza Nairobi City Stars 4-1 kwenye Uwanja wa Moi, Kasarani Jumapili.

•Mabao ya Peter Lwasa, Austin Odhiambo na Alpha Onyango yaliwahakikishia Gor Mahia taji kwa juhudi kubwa katika dakika za 63, 81 na 89 mtawalia

Wachezaji wa Gor Mahia baada ya kutawazwa mabingwa wa msimu 2022/2023.
Wachezaji wa Gor Mahia baada ya kutawazwa mabingwa wa msimu 2022/2023.
Image: TWITTER/ SPORTPESA

Vigogo wa soka nchini Gor Mahia waliibuka mabingwa mara 20 wa ligi kuu nchini FKFPL baada ya kuwalaza Nairobi City Stars 4-1 kwenye Uwanja wa Moi, Kasarani Jumapili.

Msimu huu, mabingwa hao walipata ushindani mkubwa kutoka kwa washindi wa ligi hiyo msimu wa 2021/2022, Tusker ambao walishinda mechi yao dhidi ya Vihiga Bullets mabao 4-0 katika uwanja wa Mumias Sports Complex.

Baada ya mababe hao kufungwa bao la mapema, kijibaridi kilijaa ugani huku mashabiki wa Gor Mahia wakihofia ushindi wao kuchukuliwa na Tusker ambao walikuwa tayari washawalaza Vihiga bao la kwanza.

Samuel Kapen aliifungia City Stars bao la kuongoza katika dakika ya 48 lakini Benson Omalla akarudisha usawa dakika mbili baadaye na kupelekea mechi hiyo kuwa sare kabla ya kipindi cha mapumziko.

Mabao ya Peter Lwasa, Austin Odhiambo na Alpha Onyango yaliwahakikishia Gor Mahia taji kwa juhudi kubwa katika dakika za 63, 81 na 89 mtawalia.

Baada tu ya bao la tatu kutingiza wavu, nyimbo na dansi zilisheheni uwanja mzima na pindi tu kipenga cha kutamatisha mechi kilipopigwa, mashabiki walimwagika ugani kutaka kujiunga na wachezaji katika sherehe za kuibuka mbingwa.

Sherehe hizo za kuwatawaza  zililazimika kufanyika katika jukwaa la wageni mashuhuri katika uwanja wa Kasarani kwa sababu mashabiki walikuwa wamejaa ugani.

La kusubiriwa sasa ni kama mabingwa hao watapokea hela kutoka shirikisho la soka nchini.

Ushindi huu wa Gor Mahia sasa unamaanisha wataiwakilisha Kenya katika michuano ya CAF Champions League.