Haaland avunja rekodi tatu huku Man City ikipiga Leipzig 7-0

Muhtasari

•Mabao matatu kati ya matano ya Haaland yalikuja katika kipindi cha kwanza huku akiongeza mengine mawili katika kipindi cha pili.

•Haaland alifikisha mabao 30 kwenye Ligi ya Mabingwa hivyo kumfanya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutinga hatua hiyo.

Mshambulizi Erling Halaand
Image: MAN CITY

Klabu ya Manchester City ilifuzu kwa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa baada ya kuzoa ushindi mkubwa wa 7-0 dhidi ya  RB Leipzig katika mechi ya mkondo wa pili ugani Etihad siku ya Jumanne usiku.

Mshambulizi matata wa timu ya taifa ya Norway, Erling Haaland alifunga mabao matano na kufanikisha ushindi huo wa kihistoria. Mabao matatu kati ya matano ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 yalikuja katika kipindi cha kwanza huku akiongeza mengine mawili katika kipindi cha pili.

Viungo wa kati Ilkay Gundogan na Kevin De Bruyne walifunga bao moja kila mmoja na kufunga ushindi huyo mkubwa.

Mabao matano ya Halaand katika mechi ya Jumanne usiku yalimfanya kufikisha mabao 30 kwenye Ligi ya Mabingwa hivyo kumfanya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutinga hatua hiyo.

Pia alivunja historia ya Ligi ya Mabingwa kwa kuweka rekodi ya haraka zaidi ya kufunga mabao 30.

Mshambulizi huyo pia aliibuka kuwa mfungaji bora wa Manchester City katika msimu moja huku tayari akiwa na mabao 39 msimu huu. 

Mchezaji huyo wa Norway pia ameendelea kuweka rekodi kwenye Ligi Kuu. Kufikia sasa ameweza kufunga mabao 28 huku mechi 11  zikiwa bado hazijachezwa. 

Kwa sasa anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi kwenye Uwanja wa Etihad katika msimu mmoja wa Ligi Kuu.