"Ilikuwa wakati mbaya zaidi maishani!" Ronaldo afunguka kuhusu kumpoteza mwanawe mchanga

Angél, alikufa wakati wa kuzaliwa mnamo Aprili 18, lakini pacha wake Bella alinusurika.

Muhtasari

•Ronaldo alisema yeye na mkewe Georgina Rodriguez walikuwa na matumaini kwamba mtoto wao Angél angekuwa na maisha ya kawaida.

•Ronaldo alifichua kuwa ameweka majivu ya Angél karibu na yale ya baba yake, ambaye alifariki  mwaka 2005 kutokana na matatizo ya ini.

Image: INSTAGRAM// CHRISTIANO RONALDO

Mshambulizi wa Manchester United Christiano Ronaldo amekiri kuwa kumpoteza mtoto wake mchanga mapema mwaka huu ni moja ya matukio mabaya zaidi maishani mwake.

Katika mahojiano na mtangazaji wa Uingereza Piers Morgan, Ronaldo alisema yeye na mkewe Georgina Rodriguez walikuwa na matumaini kwamba mtoto wao Angél angekuwa na maisha ya kawaida, alikiri iliwaumiza sana mtoto huyo alipofariki mnamo siku ya kuzaliwa.

"Pengine ni kumbukumbu mbaya zaidi niliyopitia maishani tangu baba yangu alipofariki. Unajua unapokuwa na mtoto  na unatarajia kila kitu kitakuwa kawaida alafu mwishowe anakuwa na shida, ni ngumu. Georgina na mimi tulikuwa na wakati mgumu sana," alisema.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno alisema kwamba yeye na mkewe walishindwa kuelewa kabisa  kilichokuwa kikiendelea na kila mara walihoji kwa nini iliwatendekea wao. Alisema kuwa familia yake iliguswa sana na matukio hayo.

Mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 37 na mkewe Georgina Rodriguez walifichua kwa huzuni kwamba mtoto wao mchanga,  Angél, alikufa wakati wa kuzaliwa mnamo Aprili 18, lakini pacha wake Bella alinusurika.

Katika mahojiano, Ronaldo alikiri kuwa alishindwa la kufanya, hakujua ikiwa alipaswa  kusherehekea kuzaliwa kwa binti yao ama kuomboleza kifo cha mwanawe.

"Sikuwahi kujua jinsi ya kuwa na furaha na huzuni kwa wakati moja. Ni vigumu kueleza. Hutaki kulia au kutabasamu kwa sababu ni jambo amblo linafanya usijue la kufanya,"

Ronaldo alifichua kuwa ameweka majivu ya Angél karibu na yale ya baba yake, ambaye alifariki  mwaka 2005 kutokana na matatizo ya ini.