Kipa wa Arsenal, David Raya akabidhiwa tuzo ya mlinda lango bora msimu wa 2023/24

Raya ameichezea Arsenal katika mechi 31 hadi sasa, na amekosa kufungwa katika mechi 16 kati ya hizo.

Muhtasari

•Raya alitunukiwa tuzo hiyo na Ligi Kuu siku ya Ijumaa, zikiwa zimesalia siku mbili tu hadi mwisho wa msimu mnamo Jumapili, Mei 19.

•‘Golden Glove’ ni tuzo ambalo hushindwa na walinda lango ambao wamecheza mechi nyingi bila kufungwa bao.

Image: TWITTER// PREMIER LEAGUE

Mlinda lango wa Arsenal David Raya amepokea rasmi tuzo la glovu ya dhahabu baada ya kuibuka mlinda mlango bora wa Ligi Kuu ya Uingereza msimu wa 2023/24.

Kipa huyo mwenye umri wa miaka 28 alitunukiwa tuzo hiyo na Ligi Kuu siku ya Ijumaa, zikiwa zimesalia siku mbili tu hadi mwisho wa msimu mnamo Jumapili, Mei 19.

Raya ameichezea Arsenal katika mechi 31 hadi sasa, na amekosa kufungwa katika mechi 16 kati ya hizo.

"Mshindi wetu wa tuzo ya Castrol Golden Glove. Hongera @davidraya,” Ligi Kuu ya Uingereza ilisema katika taarifa yake.

Klabu ya soka ya Arsenal pia imethibitisha kuwa mlinda mlango wao amepokea tuzo hiyo na kumpongeza kwa mafanikio hayo.

“Hongera sana David. Raya amekabidhiwa tuzo ya Premier League Golden Glove, inayodhaminiwa na Castrol,” Arsenal ilisema.

Waliambatanisha taarifa hiyo na picha ya Raya akiwa na tuzo hiyo huku akisherehekea pamoja na wachezaji wenzake wengine.

‘Golden Glove’ ni tuzo ambalo hushindwa na walinda lango ambao wamecheza mechi nyingi bila kufungwa bao.

Kipa huyo Mhispania alihakikishiwa kushinda ‘Golden Glove’ kwa msimu huu baada ya mpinzani wake wa karibu Jordan Pickford kushindwa kuweka cleansheet mapema mwezi huu wakati wa mechi ya Everton dhidi ya Luton Town. Pickford sasa amecheza mechi 12 bila kufungwa.

Mara ya mwisho kwa kipa wa Arsenal kushinda glovu ya dhahabu ilikuwa ni msimu wa Ligi Kuu ya Uingereza 2015/16 wakati Peter Cech alipotunukiwa tuzo hilo baada ya kutofunga mabao katika mechi 16.

Raya yuko kwa mkopo katika Arsenal kutoka Brentford kwa msimu wa EPL 2023/24. Wanabunduki hata hivyo tayari wameonyesha nia ya kumnunua kipa huyo wa Uhispania kikamilifu mwishoni mwa msimu huu.