Kocha Scott Parker atimuliwa na Bournemouth baada ya kunyukwa 9-0 na Liverpool

Cherries walinyolewa bila maji katika uwanja wa Anfield na kupoteza kwa mara ya tatu msimu huu

Muhtasari

•Parker alijiunga na Bournemouth mwezi Juni mwaka jana baada ya kukamilika kwa uhamisho wake  kutoka Fulham.

Kocha Scott Parker
Kocha Scott Parker
Image: HISANI

Bournemouth imemtimua kocha mkuu Scott Parker kufuatia kipigo cha mabao 9-0 na Liverpool  siku ya Jumamosi.

Cherries walinyolewa bila maji katika uwanja wa Anfield na kupoteza kwa mara ya tatu msimu huu tangu kupandishwa daraja kurejea ligi kuu.

Ingawa waliifunga Aston Villa siku ya ufunguzi wa msimu, pia walipoteza kwa Manchester City na Arsenal huku wakifungwa jumla ya mabao 16 katika mechi hizo.

Mwenyekiti wa Bournemouth Mxim Demin alisema, “Ningependa kuweka rekodi ya shukrani zangu kwa Scott na timu yake kwa juhudi zao wakati wa kukaa nasi. Kupanda kwetu kurejea Ligi Kuu msimu uliopita chini ya uongozi wake kutakumbukwa daima kuwa moja ya misimu yenye mafanikio zaidi katika historia yetu.''

Hata hivyo, ili tuendelee kusonga mbele kama timu na klabu kwa ujumla, ni lazima tukuwe katika mkakati wetu wa kuendesha klabu kwa uendelevu bora. Ni lazima pia tuonyeshe imani na heshima kwa wenzetu.Hiyo ndiyo njia ambayo imeiletea klabu hii mafanikio makubwa katika historia ya hivi karibuni,'' Mxim alisema.

Gary O'Neil atasimamia timu hiyo kwa muda kwa mechi ya Jumatano dhidi ya Wolves, akisaidiwa na Shaun Cooper na Tommy Elphick.

Parker alijiunga na Bournemouth mwezi Juni mwaka jana baada ya kukamilika kwa uhamisho wake  kutoka Fulham.

Kiungo huyo wa zamani wa Chelsea, Newcastle, West Ham, Tottenham na Fulham, ambaye pia aliichezea Uingereza na kushinda mataji 18, aliondoka katika klabu ya London ya kusini magharibi mwa London kufuatia kushushwa daraja kutoka kwa Ligi kuu ya uingereza.