Luke Shaw alalamika vikali juu ya uamuzi wa refa dhidi yake uliopelekea United kuadhibiwa

Shaw amekosoa uamuzi wa mwamuzi kuwapa Brighton free kick katika dakika za lala salama.

Muhtasari

•, Shaw alikiri kosa lake liliigharimu United lakini akabainisha kuwa mwamuzi Andre Marriner alifanya kosa na uamuzi wake.

•Shaw hata hivyo alisema kuwa Mashetani Wekundu wana nafasi ya kurekebisha mambo katika mechi tano za Ligi Kuu zilizosalia.

Image: HISANI

Beki wa kushoto wa Manchester United Luke Shaw amelalamika kuhusu uamuzi wa mwamuzi kuwapa Brighton free kick katika dakika za lala salama wakati wa mechi ya Alhamisi usiku kwenye Uwanja wa Amex.

Akizungumza na Sky Sports baada ya mechi hiyo ya kuvunja moyo kwa mamilioni ya mashabiki wa United, Shaw alikiri kosa lake liliigharimu United lakini akabainisha kuwa mwamuzi Andre Marriner alifanya kosa na uamuzi wake.

“Ndio, bila shaka inauma sana. Dakika ya mwisho, hatua ya mwisho kweli?,” alilalamika.

Aliongeza, "Nadhani nilipata msukumo kidogo lakini mkono haupaswi kuwa hapo. Ninalimiliki kosa langu. Ilitugharimu mchezo na ni ngumu."

Huku matokeo yakiwa 0-0 katika dakika ya 99 ya mechi hiyo ya Alhamisi usiku, Luke Shaw alionekana kumzuia Julio Enciso kukimbia kwenye eneo la hatari, na mwamuzi akatoa faulo dhidi ya beki huyo wa Uingereza. Mpira wa adhabu ulipelekea kona, ambayo iligusa mkono wa Shaw ulioinuliwa ndani ya eneo la hatari. Baada ya ukaguzi wa VAR, Brighton walipewa penalti iliyofungwa na Alexis Mac Allister.

Shaw alisema kwamba alisikitishwa na uamuzi wa Andre Marriner kutoa mkwaju wa faulo dhidi yake katika hatua za mwisho za mchuano huo mkali, uamuzi ambao alihisi uliwagharimu sana Mashetani Wekundu.

"Siwezi hata kuelezea kwa nini mkono wangu ulikuwa juu. Nilisema nilipata msukumo, labda hiyo ilisaidia kwa mkono wangu kwenda juu lakini bado haipaswi kuwa hapo. Nadhani hata kabla ya kona, mkwaju wa faulo ambao ulitolewa hapo awali haukuwa faulo," beki huyo wa timu ya taifa ya Uingereza alilalamika.

Aliendelea kulalamika, "Sitafuti visingizio lakini hakuna njia ambayo inapaswa kutolewa kama faulo inayoongoza kwenye kona hapo awali. Kwangu, labda kona hiyo haikufaa kuwepo lakini siwezi kubadili hilo.”

Shaw hata hivyo alisema kuwa Mashetani Wekundu wana nafasi ya kurekebisha mambo katika mechi tano za Ligi Kuu zilizosalia huku akibainisha kuwa lengo lao kuu ni kufuzu kwa kombe la Champions League.

Man United kwa sasa wamekalia nafasi ya nne kwenye jedwali kwa pointi 63 huku wakiwa wamecheza mechi 33.