MAELEZO: Fahamu jinsi mshindi wa Ballon d'Or anavyoamuliwa

Hafla ya Tuzo za Ballon d'Or 2024 itafanyika Oktoba 28 kwenye Ukumbi wa Theatre du Chatelet mjini Paris, Ufaransa.

Muhtasari

•Nahodha wa Argentina Lionel Messi ameshinda tuzo hiyo mara nane, huku Cristiano Ronaldo wa Ureno akiwa ndiye anayemkaribia akiwa na tuzo tano. 

•Vigezo vya tathmini ya upigaji kura vinazingatia vigezo vitatu mahususi ambavyo wanahabari wanategemea kufanya kura zao za mwisho.

walishinda tuzo za Balllon d'Or za 2023 za mchezaji bora wa kiume na wa kike wa mwaka mtawalia.
Lionel Messi na Aitana Bonmatí walishinda tuzo za Balllon d'Or za 2023 za mchezaji bora wa kiume na wa kike wa mwaka mtawalia.
Image: Ballon d'Or

Ballon d'Or ndiyo tuzo yenye heshima kubwa zaidi katika ulimwengu wa soka. Kutwaa tuzo hiyo ni ndoto ya wanasoka wengi wa kulipwa kote ulimwenguni. 

France Football, ambalo ni jarida la soka la Ufaransa ndio waandalizi wakuu wa Ballon d'Or. 

Tuzo hiyo ambayo hutolewa kila mwaka mara nyingi huhusishwa na wachezaji bora duniani huku mastaa kama Ronaldinho, Kaka, Luis Figo, Lionel Messi, Christiano Ronaldo, Michael Owen, Michel Platini, Johan Cruyff, George Weah, na Zinedine Zidane wakiwa wameishinda hapo awali.

Nahodha wa Argentina Lionel Messi ameshinda tuzo hiyo mara nane, huku Cristiano Ronaldo wa Ureno akiwa ndiye anayemkaribia akiwa na tuzo tano. 

Hafla ya Tuzo za Ballon d'Or 2024 itafanyika Oktoba 28 kwenye Ukumbi wa Theatre du Chatelet mjini Paris, Ufaransa. Hili litakuwa toleo la 68 la tuzo hiyo. 

Lakini ni nani anayeamua wateule na mshindi wa Ballon d’Or, na ni vigezo gani vinatumika? Hapa, Radio Jambo inaeleza;

Uteuzi 

Kulingana na wachapishaji wa habari za kandanda Goal.com, timu ya wahariri wa France Football, kwa ushirikiano na balozi wa Ballon d'Or na wanahabari wachache waliochaguliwa, wanaamua kuhusu orodha ya wachezaji 30 ambao watawania tuzo hiyo ya kifahari. 

Jopo la wanahabari 100 kutoka mataifa yaliyoorodheshwa kwenye 100 bora kwa soka na FIFA huchaguliwa ili kuamua mshindi. 

Uchaguzi wa mshindi 

Hapo awali, waandishi wa habari kutoka zaidi ya mataifa 180 walipewa kura na kupewa jukumu la kuchagua watano wao bora kwa tuzo ya wanaume, na kisha kura hizo zilijumuishwa na France Football kuamua orodha ya mwisho. 

Mambo, hata hivyo, yalibadilika katika toleo la 2022 wakati France Football ilipoamua kupunguza idadi ya mataifa yaliyopokea kura. Mataifa ya kushiriki yalipunguzwa kuwa 100 bora.

Mabadiliko haya yalifanyika ili kuhakikisha kuwa ni nchi zilizo na utamaduni wa soka pekee ndizo zilizohusika katika kufanya maamuzi ya tuzo hiyo ya heshima.

Chapisho la Uingereza la The Mirror linaeleza kuwa wakati wa upigaji kura, kila mwandishi wa habari hufanya chaguo lake la tano bora kutoka kwenye orodha ya wateule, huku kila nafasi ikipata pointi tofauti za kura. 

Alama sita hupewa kwa mchezaji aliyechaguliwa kwanza, kisha pointi nne kwa mchezaji aliyechaguliwa wa pili, pointi tatu kwa wa 3 aliyechaguliwa, pointi 2 kwa wa 4, na pointi moja kwa mchezaji aliyechaguliwa wa 5. 

Kisha tuzo hupewa mchezaji ambaye anapata pointi za juu zaidi katika mchakato wa kupiga kura. Iwapo zaidi ya mchezaji mmoja watalingana kwa pointi, idadi ya kura za nafasi ya kwanza walizopata hutumika kufanya uamuzi wa mwisho. 

Vigezo vya tathmini ya upigaji kura vinazingatia vigezo vitatu mahususi ambavyo wanahabari wanategemea kufanya kura zao za mwisho. Vigezo hivyo ni pamoja na;

  1. Uchezaji wa mtu binafsi katika msimu uliopita wa Agosti hadi Julai (sio kulingana na mwaka wa kalenda au mafanikio ya taaluma hata kidogo.)
  2. Mafanikio ya timu katika msimu uliopita.
  3. Tabia ya mchezaji na uchezaji wa haki katika msimu uliopita.

Vigezo hivyo vitatu humruhusu mchezaji anayecheza katika kiwango cha ustaa na kusaidia timu kushinda medali ili kupata sifa inayostahili.

Hapo awali, uchezaji wa jumla wa mchezaji ulizingatiwa na wapiga kura.

Sherehe ya utoaji tuzo;

Tuzo kuu ambazo hutolewa katika sherehe ya kila mwaka ya sherehe ni:

  • Mshindi wa Ballon d'Or kwa Wanaume kwa mchezaji bora wa kandanda wa kiume.
  • Mshindi wa Ballon d'Or kwa Wanawake kwa mchezaji bora wa soka wa kike.
  • Kombe la Kopa la mchezaji bora kijana.
  • Yashin Trophy kwa golikipa bora wa kiume.
  • Tuzo la Socrates kwa Kazi ya Kibinadamu.
  • Kocha Bora wa Mwaka.
  • Gerd Müller/Mshambuliaji Bora wa Mwaka.
  • Klabu Bora ya Mwaka.

Washindi katika vipengele mbalimbali vya tuzo hizo kwa kawaida hutangazwa kwenye tamasha la Ballon d'Or.