Maguire amsamahe MP wa Ghana aliyemkejeli naibu rais kutumia mfano wa mchezo wake duni katika Man U

Maguire alidokeza angependa kukutana na mwanasiasa huyo mcheshi kwenye uwanja wa Old Trafford hivi karibuni.

Muhtasari

•Maguire amemsamehe Mbunge wa Ghana, Isaac Adongo kufuatia matamshi ya awali ambapo alilinganisha utendaji kazi mbaya wa makamu wa rais wa nchi hiyo na mchezo wake duni.

•Adongo alibainisha kuwa nahodha huyo wa zamani wa Manchester United ameimarika sana tangu wakati huo na anacheza vyema katika klabu hiyo.

amemsamehe mbunge Isaac Adongo.
Harry Maguire amemsamehe mbunge Isaac Adongo.
Image: HISANI

Beki wa kati wa Manchester United, Harry Maguire amemsamehe Mbunge wa Ghana, Isaac Adongo baada ya mwanasiasa huyo kumuomba msamaha kutokana na matamshi yake ya awali ambapo alilinganisha utendaji kazi mbaya wa makamu wa rais wa nchi hiyo na mchezo duni wa mwanasoka huyo.

Katika kikao cha bunge cha hivi majuzi, Mbunge Adongo alibatilisha matamshi yaliyomgusia Maguire ambayo alitoa mwaka jana wakati wa kikao kingine cha bunge na kumwomba mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 30 amsamehe.

Katika hotuba yake, mbunge huyo mcheshi alibainisha kuwa nahodha huyo wa zamani wa Manchester United ameimarika sana tangu wakati huo na anacheza vyema katika klabu hiyo.

“Bwana Spika, unakumbuka kwamba mwaka jana nilikuwa mwepesi sana kumlinganisha kaka yangu mkubwa Dkt Mahamudu Bawumia na Harry Maguire. Bw Spika, sasa naomba msamaha kwa Harry Maguire,” Mbunge Adongo alisema katika kikao cha hivi majuzi cha bunge.

Aliongeza, “Mheshimiwa Mwenyekiti bwana, ulikasirika sana nilipomtumia beki wenu kama mfano. Leo Maguire amepiga kona kuwa ni mwanasoka wa mabadiliko. Maguire sasa anaifungia Manchester United mabao. Mheshimiwa Spika, Harry Maguire sasa ni mchezaji muhimu wa Manchester United."

Mwanasiasa huyo alibainisha kuwa hata kama Maguire ameimarika pakubwa, utendakazi wa makamu wa rais ambaye alilinganisha na beki huyo mwaka jana umeendelea kuzorota.

“Bwana Spika, kuhusu Maguire wetu, sasa anazurura kwenye IMF akiwa na kikombe mkononi. Kuhusu Maguire wetu, Maguire wa kiuchumi, sasa aliweza kupata wastaafu kuondoka makwao na kuja kuandamana barabarani,” Adongo alimkosoa naibu wa rais.

Naam, kwa kweli ombi la msamaha la Mbunge Adongo linaonekana kumfikia beki Harry Maguire ambaye katika maoni yake mafupi aliweka wazi kuwa amemsamehe.

Katika taarifa yake, beki huyo mwenye umri wa miaka 30 aliendelea kudokeza kutaka kukutana na mwanasiasa huyo mcheshi kwenye uwanja wa Old Trafford hivi karibuni.

“Mbunge Isaac Adongo msamaha unakubalika. Tuonane Old Trafford hivi karibuni,” Maguire alijibu kwenye mtandao wa Twitter.