Manchester United hatimaye yavunja kimya baada ya Ronaldo kuibua tetesi nzito dhidi yake

Ronaldo alilalamikia hali ya klabu hiyo na kuweka wazi kuwa hana furaha tena katika Old Trafford.

Muhtasari

•United imesema inafahamu kuhusu mahojiano hayo na kutangaza itazingatia jibu lake baada ya ukweli wote kuthibitishwa.

Ten Hag akinong'onezana na Ronaldo
Ten Hag akinong'onezana na Ronaldo
Image: The Guardinan

Klabu ya Manchester United imetoa taarifa baada ya mshambulizi wake Christiano Ronaldo kuibua madai mazito dhidi yake.

Siku ya Jumapili, mtangazaji wa Uingereza Piers Morgan aliachia mahojiano na mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno ambapo alilalamikia hali ya klabu hiyo na kuweka wazi kuwa hana furaha tena katika Old Trafford.

United imesema inafahamu kuhusu mahojiano hayo na kutangaza itazingatia jibu lake baada ya ukweli wote kuthibitishwa.

"Lengo letu linasalia katika kujiandaa kwa kipindi cha pili cha msimu na kuendeleza kasi, imani na umoja unaojengwa miongoni mwa wachezaji, meneja, wafanyakazi na mashabiki," taarifa iliyotolewa Jumatatu jioni ilisoma.

Katika sehemu ndogo ya mahojiano ya Morgan na Ronaldo, mshambulizi huyo mwenye umri wa miaka 37  alidai kuwa baadhi ya watu katika uongozi wa Manchester United akiwemo kocha Erik Ten Hag  wamekuwa wakijaribu kumtimua nje kwa nguvu tangu msimu uliopita, jambo ambalo linamfanya ahisi amesalitiwa.

"Wamekuwa wakijaribu kunitoa, sio kocha tu. Pia watu wengine watatu hivi kwenye klabu. Nilihisi nimesalitiwa," alisema.

Mshindi huyo wa Ballon d'or mara tano alikiri kuwa anahisi kusalitiwa kwani yeye ni mtu anayepaswa kuheshimiwa na kusikilizwa.

Alipoulizwa kwa nini viongozi wakuu wa klabu walikuwa wakijaribu kumfukuza, mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ureno alijibu: "Kusema kweli, sijui. Sijali. Watu wanapaswa kusikia ukweli. Ndiyo, nahisi kusalitiwa. Baadhi ya watu hawakutaka niwe hapa sio mwaka huu tu, bali mwaka jana pia."

Aidha aliweka wazi kuwa hana heshima yoyote kwa kocha wa United, Erik teg Hag,  kwani pia yeye  hajaonyesha heshima kwake.

"Simheshimu Erik ten Hag kwa sababu haonyeshi heshima kwangu. Ikiwa huniheshimu, sitawahi kukuheshimu," alisema.

Christiano pia aliibua madai kwamba hakujakuwa na mabadiliko yoyote katika klabu ya Manchester United tangu kuondoka kwa aliyekuwa kocha mkuu, Sir Alex Ferguson takriban miaka tisa iliyopita.

"Nilidhani nikirudi ningeona vitu tofauti; teknolojia, miundombinu. Kwa bahati mbaya, tunaona vitu vingi ambavyo nilizoea kuona nikiwa na miaka 21, 22, 23. Ilinishangaza sana," alisema.

Alikosoa uteuzi wa Ralf Rangnick  kama kocha wa muda baada ya kutimuliwa kwa Ole Gunnar Solskjær mwaka jana.

Christiano alijiunga tena na Mashetani Wekundu Agosti 2021 na kumaliza kama mfungaji bora wao katika mashindano yote msimu uliopita akiwa na mabao 24.