Mashetani Wekundu walambishwa sakafu na Crystal Palace huku Ligi Kuu ikielekea ukingoni

Kipigo hicho kiliweka kikwazo katika mbio za Man United za kuwania kufuzu kwa michuano ya Ligi za Ulaya msimu ujao.

Muhtasari

•United ilipokea kichapo cha aibu dhidi ya Crystal Palace kwenye Uwanja wa Selhurst Park jijini London siku ya Jumatatu usiku.

•Kiungo Michael Olise alifunga mabao mawili huku mshambuliaji Jean-Philippe Mateta na beki Tyrick Mitchell wakifunga bao moja kila mmoja.

Image: TWITTER// PREMIER LEAGUE

Timu ya kandanda ya Manchester United ilipokea kichapo cha aibu dhidi ya Crystal Palace kwenye Uwanja wa Selhurst Park jijini London siku ya Jumatatu usiku.

Vijana wa Erik ten Hag walishindwa kufunga bao lolote katika dakika tisini za mechi huku timu ya nyumbani ikifunga mabao manne dhidi ya mlinda mlango Andre Onana katika mechi hiyo isiyo ya kukumbukwa na mashabiki wa Man United.

Kiungo Michael Olise alifunga mabao mawili,  katika dakika ya 12 na ya 66, huku mshambuliaji Jean-Philippe Mateta na beki Tyrick Mitchell wakifunga bao moja kila mmoja katika dakika ya 40 na 58.

Ushindi huo uliicha Palace katika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 43, pointi moja tu pekee nyuma ya Fulham huku The Red Devils wakisalia nafasi ya nane wakiwa na pointi 54,  sawa na Chelsea ambao wako mbele kwa tofauti ya mabao.

Kipigo hicho cha Jumatatu usiku pia kiliweka kikwazo katika mbio za Man United za kuwania kufuzu kwa michuano ya Ligi za Ulaya msimu ujao zikiwa zimesalia mechi tatu tu kuchezwa.

Haya yanajiri wakati ambapo Arsenal, Manchester City na Liverpool wanachuana kileleni kuona nani atarejea nyumbani na kombe la EPL 2023/24.

Kwa sasa, Wanabunduki wanaongoza jedwali wakiwa na pointi 83, wakiwa wamecheza mchuano mmoja zaidi ya Manchester City walio nafasi ya pili wakiwa na pointi 82.

Liverpool ilijiongezea nafasi ya kusalia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania ubingwa baada ya kuifunga Tottenham wikendi. Kwa sasa wako katika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 78.