Mshambuliaji Ivan Toney akabiliwa na mashtaka 262 ya ukiukaji wa Kanuni za Kamari

Toney ameshtakiwa kwa makosa mengine 30 ya ukiukaji wa sheria za kamari za FA.

Muhtasari

•FA Ilithibitisha kwamba Toney ameshtakiwa kwa utovu wa nidhamu kuhusiana na madai ya ukiukaji wa kanuni za Kamari.

•Jumla ya mashtaka  ya ukiukaji wa sheria za FA ambayo yanamkabili IvanToney sasa imefikia 262.

Mshambuliaji wa Brentford Ivan Toney
Image: HISANI

Mshambuliaji wa klabu ya Brentford Ivan Toney ameshtakiwa kwa makosa mengine thelathini ya ukiukaji wa sheria za kamari za Football Association (FA).

Jumanne, FA kupitia kwa msemaji wake ilithibitisha kwamba Toney ameshtakiwa kwa utovu wa nidhamu kuhusiana na madai ya ukiukaji wa kanuni za Kamari.

"Mbali na shtaka la awali, inadaiwa kuwa mshambuliaji huyo wa Brentford FC alikiuka Kanuni ya E8 ya FA mara 30 zaidi kati ya 14 Machi 2017 na 18 Februari 2019," msemaji wa FA alisema katika taarifa.

Shirikisho hilo linalosimamia soka nchini Uingereza lilimpatia Toney hadi siku ya Jumatano kujibu kuhusu mashtaka hayo.

Klabu ya Brentford ilithibitisha kwamba mshambuliaji huyo amekabiliwa na mashtaka zaidi ya ukiukaji wa sheria za kamari.

"Majadiliano yetu ya faragha na Ivan pamoja na wawakilishi wake wa kisheria kuhusu suala hili yanaendelea. Ivan ana hadi Jumatano 4 Januari 2023 kutoa jibu."Brentford ilisema kutia tovuti rasmi ya klabu.

"Hatutatoa maoni zaidi katika hatua hii," Klabu iliongeza.

Jumla ya mashtaka  ya ukiukaji wa sheria za FA ambayo yanamkabili IvanToney sasa imefikia 262 baada ya mshambuliaji huyo wa Uingereza kushtakiwa kwa madai 232 ya ukiukaji wa kanuni za kamari mwezi Novemba.

Hapo awali, Toney, ambaye hakujumuishwa katika kikosi cha England katika Kombe la Dunia,  alifichua kwamba amekuwa akiisaidia FA katika uchunguzi wake kutokana na madai kwamba alicheza kamari kwenye mechi.

Mwezi Novemba, baada ya ripoti kuchapishwa magazetini  kuwa alikuwa akifanyiwa uchunguzi na  FA, alisema,  "Nifahamua habari kuhusu mimi kwenye gazeti la kitaifa leo. Nimekuwa nikisaidia Shirikisho la Soka kwa maswali yao na sitatoa maoni yoyote hadi uchunguzi huo ufikie hitimisho lake."