Mshambulizi Nicolas Jackson ajawa huzuni baada ya kocha Pochettino kutimuliwa Chelsea

Jackson ameonyesha wazi kusikitishwa kwake na kuondoka kwa kocha Mauricio Pochettino kutoka Chelsea.

Muhtasari

•Nicolas Jackson alichapisha baadhi ya kumbukumbu nzuri na kocha huyo na kuziambatanisha kwa jumbe za kihisia.

•Jackson alikiri upendo wake mkubwa kwa kocha Pochettino na kumtakia kila la kheri katika shughuli zake zijazo.

Image: INSTAGRAM// NICOLAS JACKSON

MSHAMBULIZI wa Chelsea, Nicolas Jackson, ameonyesha wazi kusikitishwa kwake na kuondoka kwa kocha Mauricio Pochettino kutoka Stamford Bridge.

Siku ya Jumanne, Mei 21, Chelsea ilitangaza kwamba makubaliano yalikuwa yameafikiwa kusitisha mkataba wa kocha huyo Mreno na klabu hiyo ya London.

Baada ya kutangazwa kwa habari hizo za kushangaza, Jackson alizamia kwenye mitandao ya kijamii ambapo alichapisha baadhi ya kumbukumbu zake nzuri na kocha huyo wa zamani wa klabu ya Tottenham Hotspurs na kuziambatanisha kwa jumbe za kihisia.

Kwenye chapisho lake la kwanza kwenye Instagram, alichapisha picha ya Pochettino akiwa ameshika shavu lake na juu yake akaambatisha emoji za mwanamume aliyeshika paji la uso wake (🤦🏻), emoji ambayo kwa kawaida hutumika kuonyesha kutamauka.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Senegal mwenye umri wa miaka 22 aliendelea kukiri upendo wake mkubwa kwa kocha Pochettino na kumtakia kila la kheri katika shughuli zake zijazo.

“Nakupenda kocha. Natamani tuendelee kuwa pamoja zaidi, lakini Mungu aendelee kukubariki wewe na familia yako,” aliandika Nicolas Jackson.

Aliongeza, "Asante kwa ushauri na sapoti. Wewe ni simba na mpiganaji wa kweli. Nakutakia kila la kheri.”