"Ni ngumu kukubali!" Bukayo Saka azungumza baada ya Arsenal kutiwa aibu na Man United

Wanabunduki walipoteza 0-2 katika dakika 90 za kawaida na pia 3-5 katika mikwaju ya penalti.

Muhtasari

•Saka alidokeza wanabunduki bado wana kazi nyingi ya kufanya ili kuwa bora zaidi kuliko walivyokuwa msimu uliopita.

•Bruno Fernandes aliwaweka mbele Mashetani Wekundu dakika ya 30 kabla ya Jadon Sancho kufunga la pili dakika 7 baadaye.

amesema Wanabunduki wana kazi kubwa ya kufanya kabla ya msimu kuanza.
Bukayo Saka amesema Wanabunduki wana kazi kubwa ya kufanya kabla ya msimu kuanza.
Image: HISANI

Arsenal walipata kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa wapinzani wao wa muda mrefu Manchester United kwenye Uwanja wa MetLife mjini New Jersey, Marekani usiku wa kuamkia Jumatatu..

Wanabunduki walipata aibu mbele ya zaidi ya mashabiki 80,000 waliokuwa wamekusanyika kutazama mechi hiyo ya kirafiki kabla ya msimu wa 2023/24 uliopangwa kuanza mapema mwezi ujao. Walipoteza katika dakika 90 za kawaida na pia katika mikwaju ya penalti, United wakifunga penalti zote tano huku Fabio Viera wa Arsenal akipiga shuti lake juu ya mtamba panya.

Wakati akizungumza baada ya mechi hiyo, winga mahiri wa Arsenal Bukayo Saka alielezea kusikitishwa kwake na mechi hiyo ya kirafiki na kukiri kwamba kipigo hicho kilikuwa kigumu sana  kukubali.

"Ni wazi kuwa ni vigumu kukubali, iwe ni mechi ya kirafiki au la dhidi ya United. Tutajifunza kutoka kwa hilo na huwezi kuruhusu mabao mawili kama hayo dhidi ya timu kama hii kwa sababu ni ngumu sana kurudi. Tunahitaji tu kujifunza kutoka kwa mechi hiyo,” Saka aliwaambia wanahabari baada ya mechi hiyo ya kukatisha tamaa.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza mwenye umri wa miaka 21 alidokeza kwamba wanabunduki bado wana kazi nyingi ya kufanya ili kuwa bora zaidi kuliko walivyokuwa msimu uliopita.

"Kimchezo tunataka kufikia kiwango ambacho tulikuwa msimu uliopita na kisha kwenda kiwango kingine na kuendelea kuongeza hiyo. Kwa busara tunahitaji kuunganisha kila mtu… Tunahitaji kuelewa mpango wetu wa mchezo na jinsi tunavyocheza na kuendelea katika kila mchezo ili tukifika kwenye mchezo wa kwanza tuwe tayari,” alisema.

Nahodha mpya Bruno Fernandes aliwaweka mbele Mashetani Wekundu dakika ya 30 ya mchuano huo baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa chipukizi Kobbie Mainoo. Mshambulizi Jadon Sancho aliongeza bao la pili takriban dakika saba baadaye na kufanya iwe vigumu kwa wanabunduki kuwashika.

Dakika 45 za kipindi cha pili zilimalizika bila bao lolote huku timu zote zikifanya majaribio kadhaa ya kutaka kufunga.

Mechi hiyo pia ilishuhudia timu zote mbili za EPL zikiwatumbuiza mashabiki wao kwa mikwaju ya penalti ambapo United ilishinda 5-3.