Sababu ya kusikitisha ya Raheem Sterling kukosa mechi ya England vs Senegal yafichuliwa

Uingereza ilitoa taarifa ikieleza kwamba alikosa mechi hiyo kutokana na masuala ya kifamilia.

Muhtasari

•Raheem Sterling hakuiwakilisha nchi yake Uingereza walipomenyana na mabingwa wa Afrika  Senegal Jumapili usiku.

•Nyumba ya mshambuliaji huyo ilivamiwa na majambazi waliokuwa na wamejihami siku ya Jumamosi

baada ya kujiunga na Chelsea kutoka Manchester City
Mshambuliaji Raheem Sterling baada ya kujiunga na Chelsea kutoka Manchester City
Image: TWITTER// CHELSEA

Mshambulizi wa Chelsea Raheem Sterling hakuiwakilisha nchi yake Uingereza walipomenyana na mabingwa wa Afrika  Senegal Jumapili usiku.

Mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 27 hakutajwa kwenye kikosi cha wachezaji 24 ambao walichaguliwa kukabiliana na Senegal, awali timu hiyo ilitoa taarifa ikieleza kwamba alikosa mechi hiyo kutokana na masuala ya kifamilia.

"Raheem Sterling hatakuwa kwenye kikosi cha Three Lions  usiku wa leo kwa kuwa anashughulikia masuala ya familia," taarifa ambayo ilitolewa na Three Lions usiku wa Jumapili ilisoma.

Ripoti sasa zimeibuka kuwa nyumba ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester City  ilivamiwa na majambazi waliokuwa na wamejihami siku ya Jumamosi. Mkewe na watoto wao walikuwa nyumbani wakati wa uvamizi huo.

Kufuatia uvamizi huo, Sterling aliomba kuruhusiwa kuenda nyumbani Uingereza ili kuwa na familia yake na  baada ya hapo ataamua iwapo atarejea nchini Qatar kuendelea na Kombe la Dunia au la.

The Three Lions wa Uingereza walipata ushindi mkubwa wa 3-0 dhidi ya Lions of Teranga wa Senegal usiku wa Jumapili. Jordan Henderson, Harry Kane na Bukayo Saka walifunga bao moja kila mmoja kufanikisha ushindi huo.

Timu ya Uingereza ilikuwa imefuzu kuingia raundi ya mwondoano baada ya kuongoza katika kundi B ambalo lilikuwa na timu zingine kama Marekani, Iran na Wales. Senagal ilichukua nafasi ya pili ya kundi A huku Uholanzi ikiongoza, Ecuador ikiwa ya tatu na wenyeji Qatar wakishika mkia.

Uingereza sasa itamenyana na Ufaransa katika hatua ya robo fainali, mchuano ambao imeratibiwa kufanyika manamo Desemba 10.