"Sijaumizwa!" Van Persie avunja kimya baada ya kushuhudia timu yake ikicharazwa mabao 9-1

Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa timu ya Heerenveen kuruhusu kufungwa mabao tisa kwenye ligi.

Muhtasari

•Aliahidi kuwa yeye na wachezaji wake wataendelea kucheza mchezo wao wenyewe na hawatapata kiwewe baada ya matokeo hayo hafifu.

•Hadi sasa ameshinda mechi moja, akatoka sare moja na sasa amepoteza mechi mbili katika msimu mpya wa ligi.

Robin Van Persie
Image: HISANI

Meneja wa Heerenveen Robin van Persie alisema alipata mafunzo mengi zaidi ya ilivyotarajiwa huku timu yake ikiweka rekodi mbaya ya kufungwa mabao 9-1 kwenye ligi ya Uholanzi mnamo Jumamosi lakini.

Hata hivyo, amebainisha kwamba hana mpango wa kubadilisha mtindo wake wa kucheza.

Akiongea na waandishi wa habari baada ya mchuano huo, mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal na Man United aliahidi kuwa yeye na wachezaji wake wa Heerenveen wataendelea kucheza mchezo wao wenyewe na hawatapata kiwewe baada ya matokeo hayo hafifu.

Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uholanzi yuko katika msimu wake wa kwanza kama mkufunzi wa klabu ya Heerenveen na katika mechi yake ya nne akiwa mkufunzi alishuhudia timu yake ikipata kipigo kikubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia yao. Aliteuliwa kuwa kocha mkuu wa Heerenveen mwezi Mei.

"Hii ni ngumu," alisema kocha huyo mwenye umri wa miaka 41.

Aliongeza, "Utakumbana na matuta kadhaa katika taaluma yako. Hili lilikuwa pigo kubwa sana. Tulijifunza masomo machache zaidi kutokana na mechi hii kuliko tulivyokuwa kawaida."

Hadi sasa ameshinda mechi moja, akatoka sare moja na sasa amepoteza mechi mbili katika msimu mpya wa ligi baada ya kuteuliwa kuwa kocha wa klabu hiyo.

Sven Mijnans alianza kuifungia AZ baada ya dakika nne pekee lakini Luuk Brouwers akaisawazishia Heerenveen katikati ya kipindi cha kwanza.

Mshambulizi wa zamani wa Tottenham Troy Parrott, 22, baadaye aliiweka timu ya nyumbani mbele kwa bao lake la kwanza akiwa na AZ tangu kuhama kwa pauni milioni 6.7 kutoka London kaskazini.

Mambo yalizidi kuwa mabaya kwa wageni mwanzoni mwa kipindi cha pili huku Parrott akiongeza mabao mengine matatu ndani ya dakika nane pekee.

Van Persie kisha alitazama timu yake ikiruhusu mabao manne zaidi katika dakika 20 za mwisho na kuipa AZ Alkmaar ushindi wao wa rekodi kwenye Eredivisie, na kuwapandisha hadi nafasi ya pili kwenye jedwali.

Ilikuwa pia mara ya kwanza kwa Heerenveen kuruhusu mabao tisa kwenye ligi na kuwaacha nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi, wakiwa na pointi nne kutoka kwa Van Persie katika michezo minne ya kwanza akiwa kocha.

“Hii ni sehemu ya soka. Sijaumizwa na hili na wala wachezaji wangu pia. Unataka kupata bora kutoka kwako mwenyewe. Hiyo inahusisha kuanguka na kuinuka tena,” Van Persie alisema.

"Hata wakati mambo hayaendi sawa, kwa kufungwa mabao matatu kwa haraka katika kipindi cha pili, ni muhimu kuendelea kufanya yale mliyokubaliana. Tutaendelea kucheza mchezo wetu. Hicho ndicho ninachokiamini na tunachokiamini,"aliongeza.

Van Persie si mgeni kwenye kipigo kikubwa kama hiki, baada ya kufungwa 8-2 na Man United wakati akiwa Arsenal mwaka wa 2011.