Klabu ya soka ya Uingereza, Luton Town imetoa taarifa kuhusu afya ya nahodha wao Tom Lockyer aliyeanguka uwanjani ghafla akicheza siku ya Jumamosi.
Ilikuwa ni wakati wa kutisha sana kwa mashabiki wa soka duniani kote wakati Tom Lockyer ,29, alipozimia katika dakika ya 65 ya mechi ya Luton dhidi ya Bournemouth kwenye Uwanja wa Vitality Stadium.
Katika taarifa yake siku ya Alhamisi, klabu hiyo iliyopandishwa daraja hadi Ligi ya Premia baada ya kufanya vyema katika michuano ya Sky Bet Champioship msimu uliopita ilidokeza kuwa Bw. Lockyer anaendelea vyema katika masuala ya afya yake na wakafichua kuwa ameanza mchakato wa ukarabati wake.
Hii ni baada ya beki huyo wa kimataifa wa Wales kuruhusiwa kutoka hospitalini na kuruhusiwa kwenda nyumbani siku ya Jumatano.
"Tunashukuru kuripoti kwamba nahodha wetu Tom Lockyer sasa ameanza kipindi cha ukarabati kutoka kwa starehe ya nyumbani kwake baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini Jumatano," klabu ya soka ya Luton Town ilisema katika taarifa.
Mechi kati ya Luton Town na Bournemouth siku ya Jumamosi ilisimamishwa mara moja katika dakika ya 65 baada ya Lockyer kuzimia uwanjani kwa njia isiyoeleweka wakati mchezo ukiendelea. Hapo hapo alipatiwa matibabu na kukimbizwa hospitali ambapo iligundulika kuwa amepata mshtuko wa moyo.
Kufuatia tukio hilo la kuogofya, mchezaji huyo wa kimataifa wa Wales mwenye umri wa miaka 29, Jumanne alipelekwa kwenye chumba cha upasuaji siku ya Jumanne ambapo aliwekewa Implantable Cardioverter Defiblillator (ICD), kifaa kinachosaidia kudhibiti tatizo la moyo.
"Klabu, Tom na familia ya Lockyer wangependa kuchukua fursa hii kurudia shukrani zetu za dhati kwa wote wa Bournemouth, wafuasi wao, viongozi wa klabu na hasa madaktari wao na kiungo Philip Billing, ambaye alikuwa wa kwanza kumfikia Tom kwenye uwanja piga na kuita usaidizi,” Luton FC ilisema kwenye taarifa hiyo.
Klabu hiyo pia imethibitisha kuwa iko mbioni kutoa huduma ya ushauri nasaha kwa wale wote ambao huenda wamepatwa na dhiki iliyosababishwa na tukio hilo.
Pia walithibitisha kuwa suala ambalo Tom alikumbana nalo siku ya Jumamosi lilikuwa tofauti na lile alilokabiliwa nalo awali.