Kipa wa Manchester United Andre Onana aliripotiwa kukasirika sana baada ya kocha wa Cameroon Rigobert Song kukosa kumjumuisha kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Guinea Jumatatu jioni.
Onana ambaye alikuwa langoni mwa Manchester United wakati ikitoa sare dhidi ya Tottenham siku ya Jumapili aliwasili Ivory Coast kwa Afcon 2023 saa chache kabla ya nchi yake kumenyana na Guinea katika mechi yao ya kwanza ya michuano hiyo.
Licha ya kufika takribani saa nne kabla ya mechi yao, mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 27 hakutajwa kwenye kikosi cha Cameroon huku kocha Rigobert Song akiamua kumchagua Fabrice Ondoa kuwa kwenye lango Jumatatu jioni.
Duru za kuaminika zimeripoti kwamba kutochaguliwa kucheza kulimkasirisha mlinda mlango huyo wa Manchester United ambaye alikuwa amesafiri takriban maili 5,000 kutoka Uingereza hadi Cameroon kiasi hadi nyota wa zamani wa Senegal El Hadji Diouf alilazimika kumtuliza.
Picha za Diouf akijaribu kumtuliza kipa huyo mwenye umri wa miaka 27 kabla ya mechi hiyo zimeendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua hisia mseto kutoka kwa mashabiki wa soka.
Inasemekana Onana alipiga kelele kwa hasira kuhusu yeye kujitolea kukodi ndege binafsi ili tu awe Cameroon kwa wakati ili kuchaguliwa kikosini kisha akakosa kuchaguliwa.
"Ikiwa sikuwa nicheze ama niwekwe kwenye timu, kwa nini nilikuja hapa kwa ndege ya kibinafsi?" Onana aliripotiwa kulalamika huku hasira zake zikizidi kupanda.
Onana hata hakuwa kwenye benchi wakati nchi yake ilipotoka sare ya 1-1 dhidi ya Guinea ambao walilazimika kukamilisha mechi hiyo wakiwa na wachezaji 10 kufuatia nahodha Francois Kamano kuonyeshwa kadi nyekundu.
Sio mara ya kwanza kwa mlinda mlango huyo wa Manchester United kutofautiana na kocha Rigobert Song. Wakati wa Kombe la Dunia mnamo Desemba 2022, alilazimika kuondoka kwenye kambi ya Cameroon nchini Qatar mapema baada ya kutofautiana na kocha.
Kipa huyo hata alipiga hatua zaidi ya kutangaza kustaafu soka ya kimataifa kabla ya kurejea kutoka kustaafu baadaye mwaka wa 2023.