Hongera! Shujaa 7s wanyakua shaba katika mashindano ya Edmonton 7s

Muhtasari

•Kenya ilichapa Canada 33-14 katika mechi ya mwisho na kumaliza katika nafasi ya tatu na pointi 16 nyuma ya Afrika Kusini na Uingereza ambao walichukua nafasi  ya kwanza na ya pili mtawalia

•Kwa sasa Kenya 7s imekalia nafasi ya tatu katika jedwali la World Rugby Series 2021 na jumla ya pointi 34 nyuma ya Afrika Kusini (40) na Uingereza (34).

Image: WORLD RUGBY SERIES

Timu ya kitaifa ya raga, Kenya 7s almaarufu kama Shujaa 7s inaendelea kuandikisha msururu wa matokeo bora kwenye mashindano ya HSBC World Rugby Sevens Series ambayo yanaendelea.

Wiki moja tu baada ya Shujaa 7s kushinda medali ya fedha katika mashindano ya Vancouver 7s, vijana wa kocha Innocent Simiyu waliweza kujinyakulia nishani ya shaba kwenye mashindano ya Edmonton 7s ambayo yalichezwa nchini Canada wikendi ambayo imetamatika.

Kenya ilichapa Canada 33-14 katika mechi ya mwisho na kumaliza katika nafasi ya tatu na pointi 16 nyuma ya Afrika Kusini na Uingereza ambao walichukua nafasi  ya kwanza na ya pili mtawalia

Shujaa 7s walikosa nafasi .ya kuhitimu kuingia fainali baada ya kupoteza 7-33 dhidi ya miamba wa raga 'The Springboks' wa Afrika Kusini kwenye mechi ya nusu fainali.

Hapo awali Kenya ilikuwa imechapa Chile 38-5, Uhispania 26-12, Ujerumani 24-17 na kupoteza tena dhidi ya Afika Kusini 14-19.

Kwa sasa Kenya 7s imekalia nafasi ya tatu katika jedwali la World Rugby Series 2021 na jumla ya pointi 34 nyuma ya Afrika Kusini (40) na Uingereza (34).