Mwanaraga mahiri wa timu ya taifa ya Shujaa 7s, Collins Injera ametangaza kustaafu kutoka kwa mchezo huo.
Jumanne asubuhi, Injera kupitia taarifa alitangaza kuwa mwili wake umezungumza naye kuwa ni wakati wa kutundika buti zake.
"Siku zote nimekuwa nikisema kwamba nitajua ni wakati, kwa sababu mwili wangu utaniambia. Na kwa miezi michache iliyopita umezungumza na mimi,hivyo hatimaye nimeamua kuisikiliza," Injera alisema.
"Ingawa hii ni ngumu kwangu, baada ya miaka 17 ya damu halisi, jasho na machozi, ni wakati wa kuondoka kwenye mchezo huu mkubwa ambao umenipa mengi zaidi kuliko yale ningeweza kuomba," aliongeza.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 alitoa shukran za dhati kwa familia yake, mkewe na watoto wao watatu (Chloe, Clyde, Carl), kwa sapoti ambayo wamempa kila wakati na kwa kuvumilia alipokuwa katika ziara ya kikazi.
"Sasa ni wakati wa mimi kuwa na wakati mzuri unaohitajika na nyinyi. Asante mama, baba na Linda kwa maombi yote, ushauri, msaada," alisema.
Injera pia aliwatambua kaka zake Humphrey Kayange na Michael Agevi ambao aliwahi kucheza pamoja nao kimataifa na humu nchini.
"Kwa wachezaji wenzangu wote, makocha, viongozi na wapinzani, asanteni kwa kumbukumbu zote tulizotengeneza uwanjani na nje," alisema.
Injera alifichua kuwa baada ya kustaafu ataendelea na kazi yake ya kihisani na pia atajiunga na biashara ya satelaiti ya Avanti Communications katika jukumu jipya la kusaidia Operesheni zake katika Afrika Mashariki.
"Kwa mashabiki wote, vyombo vya habari, wadhamini, asanteni nyote kwa sapoti katika kipindi chote cha uchezaji wangu. Natumai niliwafanya muwe na fahari," alisema.