Shujaa yajiandaa kwa mchujo wa HSBC 7s mjini Madrid,Uhispania

Timu ya taifa ya Kenya ya raga ya wachezaji saba, Shujaa, inatazamiwa kushiriki katika mchujo wa HSBC 7s kuanzia Mei 31 hadi Juni 2 mjini Madrid, Uhispania.

Muhtasari

•Kocha wa shujaa,Kevin Wambua amekitaja kikosi cha wachezaji 13,tayari kwa mechi za mchujo nchini Uhispania

•Shujaa ipo kwenye kundi moja na Samoa,Chile na wenyeji Uhispania huku timu nne zikitarajiwa kufuzu kati ya kumi na sita.

Picha;@KenyaSevens twitter
Picha;@KenyaSevens twitter

Timu ya taifa ya wachezaji 7 tayari iko mjini Madrid kwa ajili ya wikendi ambapo watawania kufuzu kwa msururu wa raga wa dunia katika mji mkuu wa Uhispania.

Kocha wa Shujaa, Kevin Wambua, aliwataja Victor Onyala na Tony Omondi kuwa manahodha wenza katika kikosi cha wachezaji 13, ambacho kinajumuisha mchezaji wa Mwamba RFC, Brian Mutua.

Shujaa watakuwa katika kundi B ambapo watamenyana na Samoa, Chile na wenyeji  Uhispania.Kocha Kelvin ‘Bling’ Wambua ataanza kampeni yake  dhidi ya Samoa saa sita na dakika ishirini na tano mchana,Ijumaa kabla ya pambano lao dhidi ya wenyeji  Uhispania saa 10:18 jioni siku hiyo hiyo.

Pambano lao la mwisho la mchezo huo ni dhidi ya Chile Jumamosi saa 8:18 usiku ambapo Shujaa wanatumai watakuwa wamejikatia tiketi ya kushiriki shindano hilo la kifahari. Mafanikio nchini Uhispania yatasaidia sana kuwapa morale baada ya kuonyeshwa vumbi kwenye mechi za mchujo za mwaka jana huko Twickenham, London ambapo walifungwa 12-5 na Canada katika fainali.

Kabla ya kuondoka kuelekea Madrid, Shujaa wamekuwa katika mazoezi ya wiki mbili huko Miramas,Ufaransa ambapo walitia nanga baada ya kampeni yao huko Munich. Timu nne kutoka kwa mchujo huu zitafuzu kwa HSBC SVNS ya 2025, inayotarajiwa kuanza baadaye mwaka huu.

Kikosi kilichosafiri:

Vincent Onyala, Tony Omondi, Kevin Wekesa, John Okoth, Brian Tanga, George Ooro, Patrick Odongo, Samuel Asati, Herman Humwa, Nygel Amaitsa, Lamec Ambetsa, Chrisant Ojwang, Brian Mutua.