Wapenzi wa raga wana kila sababu ya kutabasamu na kufurahia raga ya aina yake baada ya kuzinduliwa kwa msururu wa raga ya wachezaji saba kila upande, Sporpesa National 7s Circuit.
Katika hafla ya uzinduzi huo iliofanyika kwenye uga wa RFUEA Jumatatu asubuhi, SportPesa ilitangaza udhamini wa milioni 16.5 ambao msururu huo utajulikana rasmi kama SportPesa 7s kwa mwaka wa pili baada ya toleo la 2023 lililofanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Toleo la mwaka huu, linalotarajiwa kuanza Julai 27 (Christie 7s), linashuhudia ongezeko la ufadhili kutoka milioni 15 mwaka 2023 hadi milioni 16.5 za sasa.
Afisa mkuu mtendaji wa shirikisho la Raga nchini alieleza umuhimu wa mashindano haya katika kuendeleza utamaduni wa raga nchini.
“Msururu wa Taifa wa Raga wa SportPesa ni msingi wa kalenda yetu ya mchezo wa raga, unaotoa jukwaa la kuonesha vipaji vya hali ya juu kutoka kote nchini kwa hivyo tunakaribisha uungwaji mkono huu kwa mchezo ambao bila shaka utainua kiwango cha mashindano mwaka huu Thomas Odundo,” Afisa Mkuu Mtendaji, KRU alisema.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Kenya Harlequins Paul Murunga alionyesha utayari wa timu kabla ya mashindano hayo.
“Tumejiandaa vyema na tupo tayari kuingia uwanjani na kufanya vizuri, tumesajili wachezaji wachache kutoka klabu nyingine ambao wataiongezea nguvu timu, hatukufanya kama ilivyotarajiwa mwaka jana lakini mwaka huu wachezaji wanatazamia kufanya vyema zaidi katika toleo hili na kushinda kombe,” alisema.
Kenya Harlequin itaandaa mchuano wa ufunguzi – Christie 7s – mnamo 27/28 Julai kabla ya kuelekea Kakamega Agosti kwa KRU 7s kuandaliwa na vilabu shirikishi vya Magharibi vinavyoongozwa na Kabras Sugar.
Kutakuwa na mapumziko ya wiki moja kabla ya Kisumu kuwa wenyeji wa Dala 7s zinazopangwa kufanyika kuanzia 17-18 Agosti kabla ya Mwamba kuwakaribisha Kabeberi 7s jijini Nairobi kuanzia 24-25 Agosti.
Kutakuwa na mapumziko mengine ya wiki moja kabla ya misururu ya ya mwisho jijini Mombasa (Driftwood 7s – 7/8 Septemba) na Nakuru (Prinsloo 7s – 14/15 Septemba).