Mchezaji raga wa kimataifa wa Kenya Billy Odhiambo almaarufu Billy ‘The Kid’ ametangaza kustaafu kucheza mchezo huo ambao ameucheza kwa miaka mingi.
Billy alitangaza kustaafu kwake siku ya Jumanne asubuhi wakati alipokuwa anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya 30.
Katika taarifa kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, baba huyo wa wavulana wawili alijivunia uchezaji wake wa raga wa miaka 11 na akamshukuru Mungu kwa mafanikio yake.
"Ninapoadhimisha siku yangu ya Kuzaliwa ya 30 na kuvuka hadi muongo mpya nataka kuchukua nafasi hii kutangaza kustaafu kwangu kutoka kwa spoti ninayoipenda sana. Mungu amekuwa mwema kwangu tangu nilipovaa shati hilo kwa mara ya kwanza mwaka wa 2012 pale Port Elizabeth hadi mara ya mwisho jijini London mwaka huu. Miaka 11 njema ya Neema ya Mungu," Billy aliandika kwenye Instagram.
Mchezaji huyo mahiri ambaye katika siku za hivi majuzi amekuwa akiichezea klabu ya raga ya Mwamba pia aliithamini familia yake kwa sapoti yao kwa miaka ambayo amekuwa akicheza.
"Kwa wazazi wangu wapendwa ambao wameniunga mkono katika safari hii yote, siwezi kuwashukuru vya kutosha. Ndugu zangu Awuor ambaye pia alikuwa meneja wangu, Tim na Fiona ninawashukuru kwa kuwa kila mara kwenye kona yangu. Mke wangu ZamZam na wanangu Zafar na Zaheem ambao wamekuwa mwamba wangu, mlikuwa sehemu ya ‘kwa nini’ yangu, ninawashukuru na ninawapenda,” alisema.
Aliongeza, "Makocha wangu wote, menejimenti, washauri, wachezaji wenzangu na hata wapinzani ambao wamekuwa sehemu ya safari yangu, nawashukuru kwa kuniamini na kunifanya kuwa mtu bora. Kwenu mashabiki ambao mmesimama nami na kuniwajibisha katika safari hii yote, nawashukuru na nawapenda nyote.”
Mchezaji huyo wa raga mwenye umri wa miaka 30 amekuwa na taaluma nzuri katika mchezo huo kwa miaka 11, akishiriki mashindano 68 na kufunga majaribio 111.