logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Soka ya Ulaya imepoteza ubora mwingi, nilifungua njia ya Ligi ya Saudi- Christiano Ronaldo

"Uamuzi wangu wa kujiunga na vilabu vya Saudi ulikuwa muhimu 100% kuleta wachezaji wapya bora. Ni ukweli," Alisema.

image
na Samuel Maina

Michezo18 July 2023 - 04:25

Muhtasari


    Nahodha wa timu ya soka ya taifa ya Ureno, Christiano Ronaldo amethibitisha kuwa hatarejea tena kucheza katika bara Ulaya.

    Akizungumza katika mahojiano siku ya Jumatatu, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 38 alibainisha kuwa viwango vya soka la Ulaya vimeshuka kwa kiasi kikubwa.

    "Sitarejea kwenye soka la Ulaya, mlango umefungwa kabisa," Christiano aliwaambia waandishi wa habari.

    Aliongeza, “Nina umri wa miaka 38, pia soka la Ulaya limepoteza ubora mwingi. Ligi ya maana pekee ni Ligi Kuu (EPL), wako mbele zaidi ya ligi zingine zote."

    Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno alisifu Ligi ya Saudia ambayo anacheza kwa sasa baada ya kujiunga na Al Nassr mwezi Januari.

    Wakati wa mahojiano ya Jumatatu alijigamba kwa kufungua njia kwa wachezaji wengine wengi wakubwa ambao wanaendelea kujiunga na ligi hiyo baada yake.

    "Walinikosoa kwa kuja kwenye Ligi ya Saudi, lakini nini kinafanyika sasa?.. Nina uhakika 100% sitarejea katika klabu yoyote ya Ulaya. Nilifungua njia ya Ligi ya Saudi, na sasa wachezaji wote wanakuja hapa," alisema.

    Aliongeza, "Uamuzi wangu wa kujiunga na vilabu vya Saudi ulikuwa muhimu 100% kuleta wachezaji wapya bora. Ni ukweli.”

    ChristianoRonaldo alibainisha kuwa alipojiunga na klabu ya Juventus miaka michache iliyopita alisaidia kufufua Ligi ya Italia, Seria A ambayo kwa mujibu wake, ilikuwa imekufa.

    "Popote Christiano anaenda, yeye huzalisha maslahi ya juu," alisema.

    Pia alionekana kumshambulia kwa njia isiyo ya moja kwa moja anayeaminika kuwa mpinzani wake mkubwa, Lionel Messi kwa kusema kwamba Ligi ya Saudia ni bora zaidi kuliko Ligi ya Amerika, MLS ambayo Muargentina huyo mwenye umri wa miaka 35 alijiunga nayo mwezi uliopita.


    RADIO JAMBO FREQUENCIES

    Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


    logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved