Vilabu vikubwa vya Ligi Kuu ya Uingereza, Arsenal na Manchester United, vimemenyana katika mchezo wa kirafiki uliopigwa kwenye Uwanja wa SoFi, Jimbo la California, nchini Marekani usiku wa kuamkia Jumapili.
Mechi hiyo ya kujiandaa na msimu mpya iliyosubiriwa kwa hamu ambayo ilianza saa tisa asubuhi, masaa ya Afrika Mashariki ilishuhudia Wanabunduki wakiondoka na ushindi wa 2-1 dhidi ya mpinzani wao huyo wa muda mrefu.
Ushindi huo haukuwa rahisi kupatikanahata hivyo kwani vijana wa Mikel Arteta walilazimika kupambana kutoka nyuma baada ya mshambuliaji Rasmus Hojlund kuweka Man United mbele katika dakika ya 10.
Iliwachukua Arsenal dakika 26 kupata bao lao la kwanza kwenye mechi hiyo. Mshambulizi Gabriel Jesus aliifungia Arsenal bao la kwanza baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa chipukizi mahiri, Ethan Nwaneri.
Timu hizo mbili ziliendelea kuchuana vikali hadi Wanabunduki walipopata mafanikio katika dakika ya 81 kupitia kwa winga Gabriel Martinelli.
Mechi hiyo ilimalizika kwa Arsenal kushinda 2-1.
Hata hivyo, licha ya matokeo hayo, kulikuwa na mikwaju ya penalti ambayo Man United ilishinda kwa mabao 4-3.
Wakati wa mechi, vilabu vyote vilitoa nafasi kwa kikosi chao cha kwanza, wachezaji wa akiba na hata vijana kutoka akademi. Huenda hili lilifanywa ili kujaribu vikosi kabla ya msimu ya EPL 2024/25 unaotarajiwa kuanza mwezi ujao.
Kwa bahati mbaya, mchezaji mpya wa Man United Leny Yoro na mshambuliaji Rasmus Hojlund waliondolewa katika dakika za mapema za mechi baada ya kupata majeraha.
Katika viwanja vingine, Man City ilifungwa mabao 2-3 na AC Milan katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Yankee, New York, Marekani. Aston Villa ilifungwa 1-4 na Columbus Crew ya Marekani na Wolves ikashinda 3-1 dhidi ya West Ham katika mechi zilizochezewa Marekani pia.