The Cross-Fire, kipindi cha redio kilichoasisiwa na mkurugenzi mkuu mtendaji wa shirika la habari la Radio Africa kinarejea tena hewani Jumapili hii kwa kumbukumbu za kipekee.
Kipindi hicho ambacho kinatarajiwa kuwaunganisha washirika wote waliokifanya kuwa kipindi pendwa kuanzia mapema miaka ya 2000s kitapeperushwa moja kwa moja kuanzia majira ya saa kumi na mbili jioni katika vituo vyote vya redio chini ya mwavuli wa Radio Africa.
Mkuu wa maudhui wa shirika la Radio Africa, Paul Ilado, ambaye aliongoza kipindi hicho kuanzia mwaka 2001 kwenye kituo cha redio cha Kiss100 FM kwa mara nyingine atarejea kwa kumbukumbu nzito kwenye kiti chake.
Ilado, kama kiranja wa kipindi atawakaribisha wachangiaji mashuhuri katika kipindi hicho enzi hizo, Mukhisa Kituyi, Judy Thongori, Tony Gachoka na mtu muhimu wa wakati huo, Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Radio Africa anayeondoka, Patrick Quarcoo.
Katika kipindi hicho cha mwisho kumuaga CEO Quarcoo, Paul Ilado ataongoza kwa kuangazia kumbukumbu na safari ya dhati ambayo kipindi hicho kilijivunia ikiwa ni pamoja na mijadala mikali ambayo kwa zaidi ya miaka 20 baadae, imeunda ushiriki wa raia na maelewano kwa miaka mingi.
Kama kiranja wa kipindi, Ilado atatambulisha na kufuatilia mjadala huku wageni wetu; Mukhisa Kituyi, Judy Thongori, Tony Gachoka na mtu muhimu wa wakati huo, Patrick Quarcoo wakijadili mada tofauti kuhusu Siasa, Uchumi na zaidi.
Usikose kufuatilia kipindi hiki cha The Cross-Fire Reunion kinachorejea kwa kumbukumbu tele saa kumi na mbili jioni ya leo Jumapili ya Julai 21 kwenye stesheni zote za Radio Africa na katika matoleo ya kidijitali.