Khalwale ajiondoa kwenye kinyang'anyiro cha ugavana Kakamega, amuunga mkono Malala

Muhtasari

•Khalwale ameafikia uamuzi huo baada ya kushiriki mazungumzo na naibu rais William Ruto nyumbani kwake Karen.

•Khalwale sasa atagombea kiti cha useneta wa Kakamega, wadhfa ambao alishikilia kati ya 2013-2017.

Seneta wa zamani wa Kakamega Boni Khalwale
Seneta wa zamani wa Kakamega Boni Khalwale
Image: MAKTABA

Aliyekuwa seneta wa Kakamega Boniface Khalwale amejiondoa kwenye kinyang'anyiro cha ugavana wa kaunti  hiyo.

Khalwale ameafikia uamuzi huo baada ya kushiriki mazungumzo na naibu rais William Ruto nyumbani kwake Karen. 

Kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetangula pia walikuwepo kwenye mkutano huo uliofanyika Jumatano asubuhi.

Mwandani huyo wa Ruto sasa atamuunga mkono mgombea wa ugavana kwa tikiti ya ANC, Cleophas Malala.

Khalwale sasa atagombea kiti cha useneta wa Kakamega, wadhfa ambao alishikilia kati ya 2013-2017. Kwa sasa kiti hicho kimekaliwa na Malala.

Mnamo mwaka wa 2017, Khalwale alijaribu kiti  cha ugavana ila akalambishwa sakafu na gavana wa sasa, Wycliffe Oparanya.

Naibu rais ameeleza imani yake kwamba kaunti ya Kakamega itaunga mkono muungani wa  Kenya Kwanza.