Martha Karua atangaza kumuunga mkono Raila Odinga

Muhtasari

• Kinara wa NARC- Kenya Martha Karua hatimaye amuunga mkono Raila Odinga kwa uchaguzi wa Agosti 9.

• Hatua hii inajiri baada ya vinara wengine wa muungano wa OKA kujiunga na vuguvugu la Azimio.

Star
Star
Image: Martha Karua

Kinara wa chama cha Narc Kenya Martha Karua ametangaza kumuunga mkono kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga katika uchaguzi wa Agosti 9.

"Kutoka leo NARC- Kenya na mimi mwenyewe tunamuunga mkono Raila Odinga," Karua alisema.

Aliongeza kwamba Raila Odinga amepigania ukombozi wa taifa hili na kwamba yeye tu ndiye aliye na uwezo wa kupeleka taifa la Kenya mbele.

Aidha alisema kwamba NARC Kenya itamfanyia Raila Odinga kampeni katika maeneo yote ya taifa ili kuuza sera zake.

Karua ambaye siku ya Jumanne alitangaza kwamba muungano wa OKA ulikuwa umesambaratika hasa baaada ya vinara Kalonzo Musyoka wa Wpier, Gideon Moi wa Kanu na Cyrus Jirongo wa UDP kujiunga na muungano wa Azimio, alisema Raila ndiye kiongozi anayeweza kuliongoza taifa hili.

Akitangaza kuvunjwa kwa muungano wa OKA siku ya Jumanne, Karua alisema kwamba chama chake kingemuunga mkono tu kiongozi ambaye ana historia pana ya ukombozi wa taifa, mzalendo na muadilifu.

Kwa upande wake Raila Odinga alisema kwamba atahakikisha Karua amepata nafasi katika vuguvugu la Azimio la Umoja.

Akimtaja Karua kama kiongozi ambaye amepitia changamoto nyingi kupigania taifa hili, Raila alimpongeza kwa kufanya uamuzi mzuri kuungana naye.

Raila alisema kwamba hiyo ilikuwa fursa nzuri kwa wawili hao kuungana kwa mara nyingine  tena ili kuhakikisha wanaleta maendeleo katika taifa hili na kuwakomboa wakenya.

 

 

 

Kabla ya kukutana na Karua, kinara wa ODM Raiola Odinga alikuwa amehudhuria mkutano wa wajumbe wa chama cha UPIA.  Chama hicho kilitangaza kuunga mkono azma ya Raila Odinga.