Sabina Chege ataka Martha Karua kuwa mgombea mwenza wa Raila

Muhtasari

"Ninaomba kwamba timu yetu itamteua mwanamke katika nafasi ya mgombea mwenza, Martha Karua ana nafasi nzuri" - Sabina Chege.

Sabina Chege, mwkilishi wa kike kaunti ya Murang'a
Sabina Chege, mwkilishi wa kike kaunti ya Murang'a
Image: Facebook

Mwakilishi wa kina mama katika kaunti ya Murang’a Sabina Chege amefurahia hatua ya kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua kujiunga na vuguvugu la Azimio la Umoja na kutaja uamuzi huo kuwa wa busara na wa kujali maslahi ya mwananchi wa kawaida.

Akizungumza katika kipindi cha runinga moja nchini, Chege alimtaka mgombea urais wa muungano wa Azimio Raila Odinga kumteua Karua kama mgombea mwenza kuelekea kinyang’anyiro cha Agosti 9.

“Sisi wanawake tumepewa uongozi katika kampeni za Azimio la Umoja. Ni habari njema kwetu na kwa wanawake wote nchini Kenya. Nina hakika huu ndio muungano ambao wanawake wengi wataupigia kura. Ninaomba kwamba timu yetu itamteua mwanamke katika nafasi ya mgombea mwenza, Martha Karua ana nafasi nzuri; ni miongoni mwa wanawake wetu bora. Kwa hivyo watu wengi ambao hawajaamua watakuja ndani ya Azimio,” alisema Chege.

Kiongozi huyo wa chama cha Narc Kenya alikaribishwa Jumatano kujiunga na muungano mwa Azimio la Umoja baada ya tongoza tongoza za kisiasa za muda mrefu kutoka marengo yote miwili, ule wa Kenya Kwanza na wa Azimio la Umoja.