Uhuru anasaka kutostaafu kupitia kwa serikali ya Nusu Mkate- Mudavadi

Muhtasari

•Mudavadi amedai kuna njama kubwa ndani ya Azimio ya kumfanya Raila  kuwa Rais asiye na uwezo wa kuwa na mammlaka makuu ya kuiendesha serikali.

•Mudavadi amesema kuwa hakuna la mno ambalo serikali ya Rais Kenyatta imewafanyia wenyeji wa eneo la magharibi ili kuinua viwango vyao vya maisha

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi
Kinara wa ANC Musalia Mudavadi
Image: WILFRED NYANGARESI

Kiongozi wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi ambaye pia ni mmoja wa vigogo wakuu kwenye muungano wa Kenya Kwanza amesema kuwa Rais Uhuru Kenyatta hayuko tayari kustaafu na njama yake ya kumpigia debe Kinara wa ODM Raila Odinga kwenye muungano wa Azimio la Umoja ni njia mojawepo ya kusaka kule kusalia uongozini kupitia serikali ya Nusu Mkate.

Mudavadi ambaye aliongoza ujumbe wa Muungano wa Kenya Kwanza kwenye mkutano mkuu wa kisiasa katika kaunti ya Kakamega, alipokutana na wajumbe kutoka vyama tanzu vya muungano huo, amefichua kuwa kuna njama kubwa ndani ya Azimio ya kumfanya Raila Odinga kuwa Rais asiyekuwa na uwezo wa kuwa na mammlaka makuu ya kuiendesha serikali huku Rais Kenyatta akiwa mmoja wa wale watakaokuwa wakiiendesha serikali kupitia usiri wa mlango wa nyuma.

Mudavadi akiwa ameendamana na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetangula amewataka wenyeji wa eneo kuu la Magharibi hasa kaunti za Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia na Trans Nzoia kupuuzilia mbali msukumo wa Azimio unaoongzwa na Raila na Rais Kenyatta akisema kuwa wawili hao hawana nia ya kuwakomboa wenyeji wa magharibi hasa jamii ya Mulembe.

Akitoa mfano wa yale ambayo Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta imewafanyia wenyeji wa eneo la Kati, na kupitia “Handshake” yale ambayo yamefanyika Nyanza, Mudavadi amesema kuwa hakuna la mno ambalo serikali ya Rais Kenyatta imewafanyia wenyeji wa eneo la magharibi ili kuinua viwango vyao vya maisha akitoa mfano wa kiwanda cha kusaga sukari cha Mumias ambacho hadi wa leo hakijafufuliwa sawia na viwanda kama vile Pan Paper na pia kusisitiza kuwa miradi ya maendeleo kutoka kwa serikali ya Rais Kenyatta maeneo ya magharibi ni kama tone la maji kwenye bahari.

Kinara huyu wa ANC ambaye tangu Januari tarehe 23 alipozindua msukumo wa “Handshake” wakati wa kongamnao la wajumbe wa ANC katika ukumbi wa Bomas na akaamua yeye na Wetangula kuungana na naibu wa Rais William Ruto, amesistiza kuwa Kenya Kwanza ina nia ya kuwakomboa wakenya kutokana na hali ngumu ya kimaisha inayoshuhudiwa kwa sasa hasa kutokana na mfumuko wa bei ya bidhaa muhimu na ongezeko la gharama ya maisha likiwemo suala kuu la bei ghali ya mbolea na pembejeo za ukulima.

Mudavadi akipigia debe Kenya kwanza amesema kuwa chama cha ODM kupitia usiri wa Azimio la Umoja ulikuwa na msukumo wa kubuni chama cha DAP ili kuwahadaa wajumbe kadhaa kuegemea kwenye DAP kutokana na ODM kufifia kabisa eneo la magharibi na hasa kaunti ya Kakamega.

Semi zake zikiungwa mkono na Seneta wa Bungoma, Kiongozi wa FORD-K Moses Wetangula ambaye amewataka wenyeji wa Magharibi na Wakenya kwa jumla kumkataa kata kata Raila Odinga akimtaja kuwa kiongozi mnafiki na muongo ambaye hatimizi ahadi zake kwa wananchi na viongozi wenzake.

Wetangula amesema kuwa wana Azimio watatapatapa magharibi lakini hawataokota kura yeyote, huku akiutaja muungano wa Kenya Kwanza kama mkombozi wa wakenya.

Wetangula pia amesema kuwa kuna viongozi wanohofia kuwa iwapo Kenya Kwanza itachukua hatamu ya uongozi watalazimika kuelezea walivyofuja fedha za umma, akigusia usemi wa Mudavadi kwa magavana wa azimio alipodai kuwa walilazimishwa kuunga mkono Azimio kutokana na hofu ya kesi zao zilizo mbele ya EACC na DCI kufunguliwa kwenye faili zinazoashiria ubadhirifu na ufujaji wa mali ya umma kupitia matumizi mabaya ya mabilioni ya fedha za umma na ufisadi.

Mkutano huu pia ukitilia shime maafikiano kati ya Seneta Cleophas Malalah na Dkt Boni Khalwale yaliyoafikiwa mapema juma hili na kumpa idhini Malala kupeperusha bendera ya Ugavana na Khalwale ile ya Useneta kwenye muungano wa Kenya Kwanza kwenye kinyang’anyiro cha Agosti 9 katika kaunti ya Kakamega.

Viongozi wengine waliohudhuria wakiwapa Mudavadi na Wetangula mwanga na idhini ya kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya Kenya Kwanza ili kutetea maslahi ya watu wa magharibi na wakenya kwa jumla chini ya kauli mbiu ya Uchumi Bora, kazi ni kazi, pesa mfukoni ili kuinua maisha ya wakenya wote.

Muungano wa Kenya Kwanza unavileta Pamoja vyama vya ANC, UDA, FORD-K, Chama Cha Kazi, Tujibebe Wakenya Party, Farmers Party, The Service Party, Safina miongoni mwa vyama vingine.

Jumapili muungano huu unatarajiwa katika Kaunti ya Vihiga kwenye siku yake ya pili ya kukita kambi eneo la magharibi mwa Kenya kupigia debe Kenya Kwanza.