Usidanganywe kujiua kisiasa!- Kuria amtahadharisha Ngirici

Muhtasari

•Kuria amemtahadharisha mwaniaji huyo wa ugavana wa Kirinyaga katika uchaguzi wa mwezi Agosti kwamba amekuwa akipotoshwa na washirika wake wa kisaisa.

•Ngirici kwa upande wake amedokeza kwamba bado ataendeleza azma yake ya kuwania ugavana wa kaunti hiyo ya eneo la Mlima Kenya licha ya ushauri wa Kuria.

Moses Kuria na Purity Ngirici
Moses Kuria na Purity Ngirici
Image: KWA HISANI

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria amemshauri mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Kirinyaga, Purity Ngirici amakinike zaidi katika safari yake ya siasa.

Kuria amemtahadharisha mwaniaji huyo wa ugavana wa Kirinyaga katika uchaguzi wa mwezi Agosti kwamba amekuwa akipotoshwa na washirika wake wa kisaisa.

Kulingana na Kuria, wakazi wa Kirinyaga tayari washafanya maamuzi ya upande wa siasa ambao wataegemea katika uchaguzi wa mwaka huu.

"Kwa rafiki wangu mzuri Wangui Ngirici, sikiliza watu wako. Walishafanya maamuzi kitambo.  Usidanganywe ujiue kisiasa," Kuria alimshauri Ngirici kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Ngirici kwa upande wake amedokeza kwamba bado ataendeleza azma yake ya kuwania ugavana wa kaunti hiyo ya eneo la Mlima Kenya licha ya ushauri wa Kuria.

"Asante Moses Kuria kwa ushauri huo, hata hivyo kutokana na uchunguzi wako, inaonekana Kiambu itakuwa na Magavana watano (5) waliochaguliwa kihalali mnamo tarehe 9 Agosti 2022. Ni wazi kwamba Gavana Kabogo, Nyoro, wewe na mimi tunacheza chess wakati washindani wako wengine watatu wanacheza mpira - wawili kati yao watalazimika kuchukuliwa kwa huduma ya kwanza hivi karibuni," Ngirici amemjibu Kuria kupitia mitandao ya kijamii.

Ngirici anatazamiwa kumenyana na Gavana Waiguru (UDA), aliyekuwa Gavana wa Kirinyaga Joseph Ndathi (TSP), seneta aliye madarakani Charles Kibiru na kiongozi wa chama cha NARC-Kenya Martha Karua kwenye kinyang'anyiro hicho.