Azimio watabwagwa na UDA iwapo hawatapunguza wagombea - Herman Manyora

Muhtasari

• Herman Manyora amesema kwamba Azimio watashindwa na UDA iwapo hawatapunguza idadi ya wagombea.

• Amewataka kufaya maamuzi ya busara ili kuepuka fedheha hiyo.

Star, KWA HISANI
Star, KWA HISANI
Image: Herman Manyora

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Herman Manyora amesema kwamba huenda muungano wa Azimio la Umoja ukabwagwa na chama cha UDA katika uchaguzi wa Agosti 9, iwapo hawatapunguza idadi ya wagombea.

Akizungumza kupitia video aliyopakia katika akauti yake ya Youtube, aliwataka Azimio kubadilisha mbinu zao ili kuhakikisha wamepata ushidi katika maeneo mbalimbali nchini.

Manyora alisema kwamba uwepo wa vyama vingi chini ya mwavuli wa Azimio utasababisha kugawanya kura zao hivyo kutoa mwanya kwa UDA kuibuka kidedea.

"Unajua Azimio ina vyama vingi na watu wengi wanataka kugombea , wasipochunga na wapige hesabu zao vizuri watashindwa na UDA," Manyora alisema.

Alisema licha ya Raila Odinga kuwa na sapoti ya rais Uhuru Keyatta, anapaswa kuhakikisha wanafaya majadiliano na wagombea mbalimbali ili kuhakikisha yule ambaye ni maarufu zaidi anawawakilisha katika ngome zao.

Aidha, hakusita kuweka wazi kuwa naibu rais William Ruto ana ushawishi mkubwa katika sehemu nyingi za taifa hivyo haitakuwa rahisi kwao kumpiku.