'Pacha' wa rais Uhuru Kenyatta kuwania kiti cha Urais

Muhtasari

•Gitonga ambaye anatazamia kuwania kiti hicho cha juu zaidi kama mgombeaji huru alisema amekuwa akitafakari suala la kuongoza taifa la Kenya kwa zaidi ya mwezi mmoja.

•Aliwashambulia mafarasi wawili wakuu katika uchaguzi wa mwezi Agosti, Raila na Ruto huku akidai kwamba yeye pekee ndiye mwenye uwezo wa kuwakomboa Wakenya.

Image: FACEBOOK// MICHAEL NJOGO GITONGA

Jamaa kutoka mtaa wa Umoja  anayefanana na rais Uhuru Kenyatta kama shilingi kwa ya pili, Michael Njogo  Gitonga amejitosa rasmi kwenye siasa.

Gitonga ambaye alikuja kutambulika mwaka jana baada ya picha zake kuenezwa mitandaoni anaamini kuwa yeye ndiye bora kuridhi kiti kinachokaliwa na 'pacha' wake kwa sasa.

Akihutubia waandishi wa habari siku ya Ijumaa, Gitonga aliwashambulia mafarasi wawili wakuu katika uchaguzi wa mwezi Agosti, Raila na Ruto huku akidai kwamba yeye pekee ndiye mwenye uwezo wa kuwakomboa Wakenya.

"Sababu ya kuamua kuwa rais, nimeangalia nikaona Ruto na Raila hawawezi kusaidia watu. Wengine wanajiita hustler, mimi ni hustler halisi. Mimi ndiye nitakomboa  yule mwananchi wa chini. Najua mahitaji ya mwananchi wa chini na najua ile kazi inayomfaa," Alisema.

Gitonga ambaye anatazamia kuwania kiti hicho cha juu zaidi kama mgombeaji huru alisema amekuwa akitafakari suala la kuongoza taifa la Kenya kwa zaidi ya mwezi mmoja.

"Mimi sirudi nyuma. Huu si utani," Gitonga alisisitiza.

Gitonga atamenyana na wagombeaji wengine ambao tayari wametangaza azma yao wakiwemo Raila Odinga, William Ruto, Jimi Wanjigi, Reuben Kigame na wengineo.