Ruto atuliza joto la kivumbi cha ugavana na useneta Kisii

Muhtasari

Naibu rais ameafikia makubaliano na kiongozi mwenza Musalia Mudavadi kuteua Joash Maangi kama mgombea wa useneta kaunti ya Kisii.

Charles Matoke amelazimika kusitisha azma yake na kumuunga mkono Ezekiel Machogu.

Naibu rais William Ruto hatimaye ameingilia kati na kutoa tamko kuhusu mgombea wa Kenya Kwanza  kwenye  kivumbi cha ugavana na useneta katika kaunti ya Kisii.

Akizungumza huko Karen Nairobi, Ruto alisema kwamba amefanya mazungumzo ya kina na kinara mwenza Musalia Mudavadi ili kumpata mgombea faafu wa kuuwakilisha mrengo huo katika uchaguzi wa Agosti 9.

Mgombea wa ugavana kupitia tikiti ya  chama cha ANC, Charles Matoke aliafikia uamuzi wa kusitisha azma yake na badala yake kumuunga mkono Ezekiel Machogu wa UDA.

Akitoa taarifa yake, Matoke alisema kwamba sasa atahusika pakubwa katika kampeni za urais kuhakikisha naibu rais William Ruto anaibuka kidedea kwenye kinyang'anyiro hicho.

Kwa upande mwingine Joel Okeng'o Nyambane wa UDA alisitisha azma yake na kumuunga mkono naibu gavana wa kaunti ya Kisii, Joash Maangi [ambaye aligura chama cha ODM]  kama mgombea ambaye ataiwakilisha Kenya Kwanza kwenye kivumbi cha useneta kaunti hiyo.

"Tulikuwa na nafasi ya kuhamia vyama vingine ila hatujafanya hivyo, lengo ni kuhakikisha tunaunda chama chenye ushawishi na cha kudumu kwa miaka mingi," Okeng'o alisema.

Ruto alisisitiza kwamba kura za mchujo ndani ya chama cha UDA zitakuwa za huru na haki na kwamba atasimamia mchakato huo kisawasawa.

Viongozi hao kutoka eneo la Kisii walimhakikishia kwamba watapambana kuuza sera za Kenya Kwanza ili kuwashawishi wakazi kumchagua kama rais wao .